Header Ads Widget

RC CHALAMILA AWAKUMBUSHA WANAHABARI KUONGEZA UMAKINI KATIKA TAARIFA ZAO.


Na Matukio Daima media 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika kufikisha taarifa kwa jamii na kusaidia kujenga taifa kupitia ukosoaji wenye lengo la kujenga. 

Hata hivyo, amewataka wanahabari kuwa waangalifu na umakini zaidi katika kutoa taarifa, hasa zile zinazohusu matukio ya utekaji, na kusisitiza kuwa ni muhimu kuthibitisha usahihi wa taarifa kabla ya kuzisambaza.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika leo katika ukumbi wa Johari Rotana, Dar es Salaam, Chalamila amesema kuwa waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kuhakikisha taarifa wanazozitoa ni sahihi kwa wananchi badala ya kuleta hofu zisizo za lazima. 

Chalamila alitolea mfano tukio la mtoto aliyeripotiwa kutekwa, ambapo taarifa zilienea kwa kasi na kuchochea hofu kubwa miongoni mwa jamii, hata hivyo ilibainika baadaye kuwa mtoto huyo alikuwa ameanguka kisimani na siyo kutekwa kama ilivyodaiwa awali.

Rc Chalamila pia, alitolea mfano tukio la mfanyabiashara Daisle Simon Ulomi, ambaye aliripotiwa kupotea kwa madai ya kutekwa, huku baada ya uchunguzi wa polisi, ilibainika kuwa Ulomi alipata ajali ya pikipiki na kupoteza maisha, na mwili wake ukihifadhiwa kama mtu asiyefahamika (unknown) kwa sababu hakuwa na kitambulisho chochote.

Aidha, Chalamila amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya usalama, hasa katika kipindi cha sikukuu, ili kudumisha amani na usalama. 

Amesema kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa salama wakati wote, na kwamba wanahabari wanapaswa kuungana na vyombo vya usalama katika kusambaza taarifa sahihi na zenye manufaa kwa jamii.

Mkuu huyo wa Mkoa pia amewakumbusha wananchi kuwa na tabia ya kutembea vitambulisho, akisema kuwa ni muhimu katika kusaidia utambuzi wa raia hasa wakati wa matukio ya dharura. 

Pamoja na hayo, RC Chalamila alitoa onyo kali kwa wale wanaosambaza uvumi na taarifa zisizo na msingi, amesema kuwa taarifa za uongo au zisizo sahihi zinaweza kusababisha hofu isiyokuwa ya lazima na kuathiri hali ya usalama wa jamii kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI