Na,Jusline Marco:Arusha
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha imeahidi kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuhakikisha wanapanua wigo wa kushiriki kwenye sekta ya utalii katika kutangaza vivutio vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, katika uzinduzi wa kampeni ya Msimu wa Sikukuu Ngorongoro,Katibu Tawala Msaidizi,Huduma za Uchumi na Uzalishaji mali Mkoa wa Arusha Daniel Loiruku amesema uzinduzi huo umelenga kutangaza utalii ndani na nje ya Mkoa wa Arusha.
Loiruku amesema kuwa katika kumaliza mwaka 2024 na kuanza mwaka 2025 mipango na mikakati iliyoboreshwa ipo mbioni kwa ajili ya kuanza kutekelezwa rasmi ambayo ni fursa muhimu kuhakikishia umma wa Watanzania kuweza kutumia ili kufikia malengo na kukuza utalii utakaosaidia kuongeza mapato na kuboresha mambo mbalimbali.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Dawati la Huduma za Utalii na Masoko kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Mariam Kobero katika uzinduzi huo amesema kampeni hiyo ambayo imeanza leo Disemba 4 itafikia ukomo Januari 4 ,2025 ambapo amesema lengo la kampeni hiyo ni kuwezesha watanzania kuweza kutembelea hifadhi ya Ngorongoro.
Kampeni hiyo yenye kauli mbiu ya Merry and Wild Ngorongoro Awaits, ni kampeni inayotekeleza shughuli za Utalii kuelekea mwisho wa mwaka kwa lengo la kuwahamasisha watanzania kutembelea vivutio vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo.
Ameeleza kuwa kwa sasa idadi ya watalii wa ndani inazidi kuongezeka hali ambayo NCAA imeona kuwa inajukumu la kuendelea kuhamasisha watalii ili waweze kutumia msimu huo kutembelea hifadhi hiyo na kuweza kujionea vivutio ambavyo vipo na baadhi ya watalii hawajaweza kuviona.
Katika hatua nyingine Kamishna Mariam ameeleza kuwa katika utekelezaji wa kampeni hiyo NCAA itashirikiana na Kampuni ya Smile Safari ya jijini Arusha na kuwatumia vijana maalum wajulikanao kama Action Rollers Skates ambao watakuwa katika mitaa mbalimbali kwenye mikoa ya Arusha,Dar es salaam pamoja na Zanzibar kuanzia Disemba 4 hadi 16 mwaka huu.
Vilevile NCAA imeainisha aina ya viingilio na gharama ambazo zitatumika katika kampeni hiyo ikiwemo kiingilio cha Faru,Tembo na Chui vikijumisha kiingilio,chakula,muongoza utalii usafiri na huduma ya picha.
Sambamba na hayo amesema katika kuelekea msimu wa Ndutu kutokana na eneo hilo kuwa maarufu kwa mazilia ya Nyumbuhivyo ni fursa kwa watanzania kufahamu eneo hilo na umuhimu wake.
0 Comments