Na Moses Ng'wat, Songwe.
MWANAUME ambaye utambulisho wake haujafahamika na anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 hadi 30, ambaye anadaiwa kuwa ni mtuhumiwa wa wizi wa Pikiki ameuawa na wananchi, kisha mwili (maiti) yake kufungwa kamba na kuburuzwa nyuma ya pikipiki.
Taarifa iliyotolewa leo Disemba 7, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo aliuawa na wananchi wenye hasira Disemba 6, 2024 katika Mtaa wa Nazareth, Kata ya Mwakakati, Mjini Tunduma, Wilayani Momba.
Taarifa hiyo imesema mtuhumiwa huyo, aliuawa kwa kupigwa na silaha za jadi, kisha mwili wake kufungwa kamba kwenye pikipiki na kuanza kuburuzwa na wananchi wenye hasira kali.
Taarifa hiyo ya Kamanda wa Polisi imefafanua zaidi kuwa, mwanaume (mtuhumiwa) huyo aliuawa na wananchi hao wakimtuhumu kuiba Pikipiki maeneo hayo.
Hata hivyo, jeshi hilo limeeleza kuwa linaendelea na upelelezi ukiambatana na msako mkali wa kuwatafuta wahusika waliofanya tukio hilo.
Aidha, linatoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi ili kuepusha kutokea kwa matukio mabaya kama hayo ya mauaji.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limetoa taarifa ya tukio lingine la kufariki dunia, Oscar Mwampashi (41), Mkazi wa Kitongoji cha Nselewa, Kata ya Mlowo, Wilayani Mbozi, baada ya kupigwa na radi akiwa anachunga Ng'ombe.
Taarifa imesema kuwa tukio hilo lililotokea Disemba 06, 2024 na kwamba Marehemu alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mbozi Mision alikopelekwa baada ya kupatwa na tukio hilo.
0 Comments