Header Ads Widget

HUDUMA YA WAHURUMIENI CHINI YA MWAMVULI WA AGIVA YAZIDI KUWASAIDIA WENYE UHITAJI ARUMERU.

Na,Jusline Marco:Arusha

Wazee wasiona zaidi ya 80 walio katika kituo cha Agape Blind kilichopo kijiji cha Nambala Kikwe Wilayani Arumeru wamepatiwa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo vyakula na mavazi kutoka Kikundi cha AGIVA kupitia Huduma ya Wahutumieni.

Msaada huo ambao umekuwa ukitolewa na Kikundi hicho umekuwa ukiwafikia wahitaji wengi ndani ya Mkoa wa Arusha ikiwemo wajane,watoto yatima na waishio kwenye mazingira magumu,walemavu wa viungo na wasiona ikiwa ni moja ya jitihada za kuunga mkono serikali ya awamu ya sita kwa kuwafikia wahitaji hao ambao serikali haijaweza kuwafikia.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa mahitaji hayo mmoja wa waanzilishi wa kikundi hicho Bi.Agnes Mayagila amesema kikundi hicho kimekuwa kikitembelea vituo mbalimbali na kutoa sadaka zao kwa kushirikiana na jamii inayoguswa na huduma hiyo.

Ameongeza kwa kuwaomba wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi hizo kwani wapo wahitaji mbalimbali katika jamii ambao kwa namna moja ama nyingine serikali haijafanikiwa kuwafikia hivyo ameomba kupitia huduma ya Wahurumieni,wadau mbalimbali na watu wenye moyo wa kusaidia wajitokeze kusaidia wahitaji hao.

Ameeleza kuwa huduma ya Wahurumieni inaendeshwa kwa imani ya Kristo Yesu ambapo pamoja na sadaka wanazotoa ni matamanio yao watu wamjue Mungu na kumtegemea ili azidi kugusa mahitaji yao na kugusa wengine kuweza kuwasaidia.

Naye Vaileth Danien mwanzishili mwenza wa kikundi hicho amesema utoaji wa msaada huo imekuwa ni desturi yao katika kurudisha fadhila kwa jamii yenye uhitaji kwa kile walichokipata kwa kushirikiana na jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Agape Blind Gietrick Kristomkomba Ambazipi amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ni kusaidia wahitaji hao ambao hawakuwa na mahali pa kuishi ikiwa ni sambamba na kusomesha watoto wao.

Mbali na hayo Bwn.Ambazipi amesema kituo hicho kilianzishwa mnamo mwaka 2007 ambapo mpaka sasa kituo hicho kinajumla ya watu wasioona 83 wakiwemo watu wazima na watoto kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza,Shinyanga,Tabora,Zanzibar na Singida.

Aidha ameiomba serikali kuendelea kuunga mkono juhudi za watu ambao wamejitoa kusaidia wenye uhitaji kwa malazi,chakula na hata kimatibabu ambapo pia amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa watoto wao kwaajili ya vizazi vijavyo.

Pamoja na hayo amebainisha baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo kuhifadhi baadhi yao pindi wanapofariki maana wengi wao hawana ndugu,kukosa fedha za kusomesha watoto wao elimu ya juu huku wakati mwingine kukosa chakula kwani kituo jicho kimejikita kwaajili ya kuwapa hifadhi pekee.

Mmoja wa wazee hao wasiona akizungumza kwa niaba ya Wanzake amekishukuru kikundi hicho kupitia huduma ya Wahurumieni kwa kuguswa na kufika kwao kuwasaidia.




 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI