Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Biashara yenye thamani ya dola milioni 209.8 za Marekani imefanyika kati ya Tanzania na Burundi tangu kuanzishwa kwa vikao vya ujirani mwema baina ya mkoa Kigoma na mikoa sita ya Burundi mwaka kuanzia 2004 hadi mwaka 2023.
Mkurugenzi wa biashara, uwekezaji na sekta za uzalishaji kutoka wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Benjamen Mwesiga alisema hayo katika maadhimisho ya miaka 20 ya kuanzishwa kwa vikao vya ujirani mwema baina ya mkoa Kigoma na mikoa ya Burundi inayopakana na mkoa Kigoma.
Mwesiga alisema kuwa kufanyika kwa vikao hivyo kumewezesha kufanyika kwa majadiliano mbalimbali na changamoto zilizokuwa zinajitokeza katika masuala ya usalama, vikwazo vya kibiashara vya kuvuka mpaka, vibali na masuala mazima ya uchumi na biashara hivyo kuwezesha changamoto nyingi kufanyiwa kazi.
Kutokana na hilo Mwesiga alisema kuwa Tanzania imeongeza mpango wa kufanya biashara na Burundi ikiwemo kuanzisha safari za ndege mara tatu kwa wiki kutoka Dar es Salaam kwenda Bujumbura, kuwezesha asilimia 95 ya mizigo ya Burundi kupitishwa bandari ya Dar es Salaam ambapo kwa sasa tayari umesainiwa mkataba ambao utawezesha kujengwa kwa reli ya kisasa kutoka Uvinza mkoani Kigoma nchini Taanzania hadi Gitega nchini Burundi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Vikao vya ujirani mwema ambaye ni Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema kuwa kufanyika kwa vikao vya ujirani mwema ambavyo msingi wake ulikuwa kujadili masuala ya ulinzi na usalama kumewezesha kuingizwa kwa ajenda ya kiuchumi.
Katika hilo Mkuu huyo wa mkoa Kigoma alisema kuwa vikao hivyo kwa kipindi hicho cha miaka 20 vimewezesha kujengwa kwa masoko sita ya ujirani mwema maeneo ya mpakani ambayo yanatumika kufanyika biashara kwa Pamoja baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Burundi huku akibainisha kuwa serikali ya Raisi Samia Suluhu Hassan imeupatia mkoa Kigoma shilingi Trilioni 11.9 ambazo zinaufanya mkoa kuwa kitovu cha biashara na uchumi kwa ajili ya nchi za maziwa Makuu ikiwemo biashara na Burundi
Muasisi mwenza wa vikao hivyo Mkuu wa mkoa Mstaafu wa Makamba nchini Burundi, Reverien Ndikuriyo ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa cha tawala cha CNDD-FDD cha nchini Burundi alisema kuwa kudhibitiwa kwa vitendo vya ujambazi na uhalifu wa kutumia silaha ukihusisha uhalifu wa kuvuka mpaka umewezesha maeneo hayo kuwa salama na shughuli za uchumi na biashara kufanyika kwa tija.
Ndikuriyo alisema kuwa kwa sasa Tanzania na Burundi zina uhusiano mkubwa wa kihistoria na kindugu ambapo kwa siku za karibuni Burundi inatarajia kufanya uwekezaji mkubwa kwenye viwanda na Biashara
0 Comments