WATU 7 wamefariki dunia na wengine 9 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu katika kijiji cha Kihanga wilaya ya Karagwe mkoani Kagera
Kamanda wa jeshi la Polisi mkoani Kagera, Blasius Chatanda wakati akiongea na waandishi wa habari amesema ajali hii imetokea Desemba 3 majira ya Saa Tano asubuhi mwaka huu na kuhusisha magari matatu ambayo ni scania no T621EJQ ikiwa na Trailer no T472 EAQ likitokea Kayanga wilayani Karagwe kwenda Kyaka wilaya ya Missenyi mkoani Kagera na kugonga magari mawili ya abiria ambayo ni Costa no T367 ECP na Hiace no T976 DGD yaliyo kuwa yamesimama katika eneo hilo kwa ukaguzi wa idara ya uhamiaji
Kamanda Chatanda amesema ajali hiyo imesababisha vifo vya watu saba wanawake 4, watoto wawili na mwanaume mmoja pamoja na majeruhi 9, wanawake 5 na wanaume 4 huku akitaja chanzo cha ajali hii kuwa ni uzembe mkubwa wa dereva aliyekimbia baada ya ajali hiyo na kusema kuwa ajisalimishe kabla jeshi la polisi halitamkamata
Kufuatia tukio hilo Chatanda ametoa pole kwa wafiwa wote na kuwataka madereva kuzingatia sheria kanuni na taratibu wawapo barabarani na kueleza kuwa majeruhi wamepelekwa katika hospitali ya wilaya ya Karagwe kwa matibabu zaidi.
0 Comments