Header Ads Widget

WAKULIMA DODOMA WANUFAIKA MAFUNZO YA MATUMIZI YA NISHATI YA UMEME JUA KWA UMWAGILIAJI.


Na Hamida Ramadhan Matukio Daima app Dodoma


WAKULIMA wadogowadogo wa kijiji cha Matumbulu, kata ya Matumbulu mkoani Dodoma, wamepewa mafunzo ya kisasa kuhusu matumizi ya nishati ya umeme jua kwa shughuli za umwagiliaji.


Mafunzo haya yameandaliwa na Taasisi ya African Centre for Media Excellence (ACME) ya nchini Uganda yanayo lenga kusaidia wakulima kuboresha tija katika kilimo chao kwa kutumia mbinu za kisasa.


Kwa muda mrefu, asilimia 90 ya wakulima hawa wamekuwa wakitegemea visima na mabwawa yanayotumia pampu zinazotumia mafuta ya dizeli na petroli, hali ambayo imekuwa ikiathiri uzalishaji kutokana na gharama kubwa za mafuta, katika mafunzo haya, wakulima wamepewa elimu ya namna ya kutumia nishati ya umeme jua kwa gharama nafuu zaidi, ikiwa ni mbadala wa mafuta.


Marry Mabwahi, mkulima wa nyanya na zabibu kijijini hapo, anasema anatamani kutumia nishati ya umeme jua kwenye kilimo chake, lakini changamoto kubwa ni gharama za vifaa vya umeme jua.


 “Ombi letu kama wakulima ni kupunguziwa gharama ili na sisi wa hali ya chini tuweze kutumia na kunufaika na kilimo chetu,” amesema Marry. 


Na kuongeza kuwa"Leo tumepewa wazo la kujiunga kwenye vikundi vya ushirika ambavyo vinaweza kuwasaidia kupata mikopo ya kununua vifaa vya umeme jua.



Kwa upande wake, Melea Benjamin,mkulima ambaye analima zabibu, mahindi, na nyanya, ameeleza kuwa amekuwa akitumia umeme jua kwa matumizi ya nyumbani. 


“Kupitia elimu tuliyopata, tumejifunza kuwa nishati ya umeme jua inaweza kutumika pia kwenye kilimo kwa shughuli za umwagiliaji na hivyo kuongeza uzalishaji wetu,” amesema Melea. 


Na kuongeza "Sasa nakusudia kujiunga na vikundi vya ushirika ili niweze kupata mkopo wa vifaa vya umeme jua na kuendeleza kilimo cha kisasa, " Amesema


Maoni ya Maafisa wa Kilimo na Taasisi za Mafunzo


Afisa Kilimo wa kata ya Matumbulu, Aneth Mnana, anabainisha kuwa katika eneo lake muitikio wa wakulima kulima kwa kutumia nishati ya umeme jua ni hafifu wengi wanalima kilimo cha kizamani wanamwagilia kwa kutumia visima na mabwawa yanayoendeshwa kwa pampu zinazotumia Mafuta ya Dezel na Petrol .


Lakini pia anasema kuna baadhi ya wakulima walioanza kutumia umeme jua wameanza kuona faida, hasa kwenye kilimo cha bustani ambapo mazao kama nyanya, vitunguu, na pilipili hoho yanawanufaisha. 


Amesema kuwa eneo la kilimo cha mazao ya chakula ni takribani hekta 300, zabibu hekta 500, na kilimo cha mbogamboga hekta 10.



Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi Don Bosco Dodoma, Dkt. Justine Mlebyia, alisema kuwa chuo hicho kimejikita kuzalisha wataalamu wa nishati ya umeme jua kwa shuguli za kilimo. 


“Tunalenga kuhamasisha vijana na wakulima wengine kuangalia kilimo kama fursa, na si adhabu kwani ni muhimu kutumia nishati ya umeme jua ili kuongeza tija katika maeneo yenye changamoto ya maji kama Dodoma,” alisema Dkt. Mlebyia.


Hata hivyo Mafunzo haya yanatoa matumaini mapya kwa wakulima wadogo Dodoma, ambapo pamoja na changamoto za gharama, wakulima wanaanza kuelewa umuhimu wa nishati ya umeme jua katika kilimo. 


Kwa kujiunga kwenye vikundi vya ushirika, wanaweza kupata fursa za mikopo kupitia taasisi za kifedha zinazoshirikiana na makampuni ya usambazaji umeme jua, hivyo kusaidia kuimarisha sekta ya kilimo Dodoma na kuinua hali za wakulima wadogo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI