Na Moses Ng'wat, Songwe.
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) Kata ya Ikana, Wilayani Momba, Amos Sikamanga (41) amelazwa katika kituo cha afya Tunduma akidaiwa kujeruhwa vibaya kwa kuchomwa kisu cha utosi na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Tukio hilo limetokea Novemba 27, 2024 majira ya 3:00 asubuhi katika eneo la kituo cha kupigia kura cha Nakawale katika kijiji cha Nakawale, Katani hapo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Momba, Chuki Sichalwe, amesema Mwenyekiti huyo alijeruhiwa kwa kuchomwa na kisu kichani sehemu ya utosi alipofika katika kituo hicho cha kupigia kura cha Nakawale kwa lengo la kukagua Mawala wa chama hicho wakati zoezi la kupiga kura likiendelea.
"Viongozi hao wa Chadema walikuwa wanamzuia Mwenyekiti wetu asiingie kwenye chumba cha mawakala wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ofisi hivyo kuzuka vurugu zilizosababisha kuchomwa kisu" Alifafanua Sichalwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari linawashikilia viongozi wawili wa Chadema juu ya tukio hilo.
Kamanda Senga aliwataja viongozi hao wa Chadema wanaoshikiliwa ni Gidion Siame (34) ambaye ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Momba na Fiston Haonga (57) ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee (Bazecha) Jimbo la Momba wote wakazi wa kijiji cha Nakawale Wilayani humo.
Akifafanua zaidi Kamanda Senga alisema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha tukio hilo ni mihemuko ya kisiasa ambapo watuhumiwa walikuwa wanamzuia mhanga asiingie kwenye chumba cha mawakala wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ofisi ya Kijiji cha Nakawale.
"Mhanga yupo Kituo cha Afya Tunduma anaendelea na matibabu na uchunguzi wa tukio hili bado unaendelea na pindi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani" alifafanua zaidi Kamanda Senga.
0 Comments