Na Fadhili Abdallah,Kigoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma kimesema kuwa kimefanikiwa kushinda vijiji 293 kati ya vijiji 306 vilivyofanya uchaguzi mkoani Kigoma huku vyama vya upinzani vikifanikiwa kushinda vijiji 13 tathmini inayoelezwa chama hicho kushinda kwa asilimia 96 mkoani Kigoma,
Katibu wa siasa,uenezi na mafunzo wa CCM mkoa Kigoma, Deogratius Nsokolo alisema hayo akitoa taarifa ya tathmini inayoonyesha viti ambavyo chama hicho kimeshinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 17 mwaka huu.
Nsokolo alisema kuwa katika uchaguzi huo CCM imeshinda mitaa 170 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na wilaya Nzima ya Kasulu kati ya mitaa 176 iliyoshiriki uchaguzi huo ambapo katika manispaa ya Kigoma Ujiji upinzani umepata viti viwili vya uenyekiti na viti vinne kwenye Halmashauri ya Kasulu.
Katibu Mwenezi huyo wa CCM mkoa Kigoma alisema kuwa katika nafasi ya wenyeviti wa vitongoji CCM imeshinda vitongoji 1716 kati ya 1858 na wapinzani wameshinda vitongoji 140 ambapo vitongoji viwili bado uchaguzi ambao umerudiwa jana matokeo yalikuwa hayajatangazwa.
Akizungumzia matokeo yaliyotangazwa Katibu wa ACT Wazalendo mkoa Kigoma, Rashidi Yunus Ruhonvya alisema kuwa CCM imeshinda kwa kura nyingi lakini hiyo inatokana na kuendesha uchaguzi kwa kutegemea dola hivyo ushindi wa CCM umepatikana kwa kupitia dola badala ya kutumia njia ya Demokrasia.
Ruhonvya alisema kuwa tathmini waliyofanya inaonyesha ACT Wazalendo kushinda vijiji 207 kati ya vijiji 306 lakini wagombea wao licha ya kushinda hawakutangazwa na ambapo ametaja maeneo waliyotangazwa kuwa ni pamoji na mwenyekiti wa kijiji kimoja na vitongoji vitatu Kasulu Vijijini, mtaa mmoja Kasulu Mjini, Kakonko wakipata wenyeviti wa vitongoji vitano na Wenyeviti wa vitongoji saba katika jimbo la Kigoma Kaskazini.
Omari Gindi ni Mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Kigoma Mjini alisema kuwa wamesikitishwa na serikali ilivyosimamia uchaguzi kwa kutumia vyombo vya dola kufanya kila aina ya kuharibu uchaguzi na hivyo kutoa nafasi ya wagombea wa CCM kupata ushindi.
Gindi alisema kuwa walikuwa na jumla ya wagombea 52 nafasi ya wenyeviti wa mitaa na wajumbe 193 ambapo wagombea wao walienguliwa na kubaki wenyeviti 31 na wajumbe 36 ambapo baada ya uchaguzi mgombea wao mmoja ndiyo ametangazwa kushinda nafasi ya Mwenyekiti wa serikali ya mtaa na wajumbe wawili kwa manispaa nzima ya Kigoma Ujiji.
Mwisho.
0 Comments