Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma.
WAZIRI wa Fedha Dkt, Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali ina imani kubwa na sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya nchi ikiwemo huduma za Benki kwani zimeendelea kufanya vizuri na kuwa na mchango mkubwa katika kuchagiza kukua kwa uchumi na kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Ametasema hayo leo jijini hapa kwenye Hafla ya uzinduzi wa hatifungani inayofahamika kwa BONDI YANGU inayoendeshwa na Azania Benki.
Amesema Kwa kutambua mchango mkubwa wa Sekta ya Fedha katika maendeleo na kukua kwa uchumi Serikali imekuwa ikiweka juhudi katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya kisera na kisheria katika kuwezesha ustawi wa Sekta ya Fedha katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na benki, bima, masoko ya mitaji na dhamana, mifuko ya uwezeshaji na mengineyo.
"Kwa upande wa Benki, huduma hizi zimeendelea kuongezeka hapa nchini kama inavyojidhihirisha kwa kuwapo kwa huduma na bidhaa mbalimbali za benki ambapo Ubora wa huduma na mali katika sekta ya benki umeendelea kuongezeka ikiwa ni pamoja na kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu, " Amesema
Aidha amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wetu wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan iliandaa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali Mkakati wa Kugharamia Miradi ya Maendeleo kwa njia Mbadala (APF) ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21-2029/30 ambapo miongoni mwa malengo yake ni kuhakikisha Taasisi mbalimbali zinatumia vyanzo bunifu na mbadala ambavyo vipo na vina uwezo wa kutoa mitaji.
Mkakati huo ulizinduliwa rasmi Mei 2021. Vyanzo hivyo mbadala ni pamoja na Hatifungani za aina mbalimbali ikiwa pamoja na za kijani, bluu na nyingine za aina hiyo, matumizi ya mitaji halaiki (crowdfunding), kutafuta mitaji kupitia masoko ya hisa (equity financing), PPP, Hatifungani za Miundombinu (Infrastructure Bond), Hatifungani za Mamlaka za Serikali za Mitaa (Municipal Bonds); Lease Financing; Diaspora Bonds; na nyinginezo.
"Nimetaarifiwa na kushuhudia jinsi Benki ya Azania ambavyo mmekuwa mkifanya vizuri kila siku katika kutoa huduma za kibenki sehemu mbalimbali na kupitia njia mbalimbali, " Amesema
Na kuongeza "Na sasa mmetuonesha nia yenu nzuri ya kuongeza chachu ya maendeleo kwa Taifa na kuiunga mkono serikali kwa kutoa mchango wenu katika kufanikisha mipango mbalimbali ya kimkakati na hasa ushirikishwaji wa kifedha kwa vikundi vya kinamama na vijana kupitia fedha zitakazopatikana kwa mauzo ya hati fungani hii, " Amesema Dkt Mwigulu
Amesema kwamba kwa miaka mingi, Benki ya Azania imekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma mbalimbali za kibenki kwa vikundi mbalimbali na mradi huu ni katika kuimarisha utoaji wa huduma zenu kwa makundi yaliyo nje ya wigo wa kibenki.
"Naamini makusanyo ya hati fungani hii yataleta chachu kubwa katika kuwawezesha wale ambao wanakwama kupata huduma rasmi za kibenki kuwezeshwa kiuchumi kama tunavyotambua kutokana na tafiti mbalimbali idadi ya watu wazima wanaotumia huduma za kibenki ni takriban asilimia 22 hivyo jitihada hizi za kukusanya fedha kupitia hati fungani hii zitatoa fursa kwa vikundi vya kinamama na vijana kupata mikopo nafuu itakayowakwamua kiuchumi, "amesema.
Na kuongeza "Nimeona viwango vya riba vya Hati Fungani hii ni rafiki sana kwa mtanzania hata yule mwenye kipato cha chini kuweza kumudu, Shilingi 500,000 tu kwa riba ya asilimia 12.5 kwa mwaka, na unapata gawio la faida kila baada ya miezi mitatu, hii inaonesha mna nia ya dhati katika kumkomboa mtanzania, hongereni sana, "
"Hii ni tofauti na hatifungani nyingi zinazotoa gawio la faida kila miezi sita (6). Pia hata ukomo wa miaka minne (4) ni muda rafiki wa uwekezaji Hongereni sana kwa ubunifu huu ambao utafungua njia kwa wengine kufuata nyayo zenu, " Amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Azania Benki Dkt, Esther Mang'enya Amesema mwaka 2023 ulikuwa ni mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa malengo mkakati wa Azania Benki na Benki ilifanikiwa kupata matokeo chanya.
" Tuliweza kukuza Mizania kufika Trioni 2.3 na kutengeneza faida ya Bilioni 29 na kuongeza gawio la billioni 8.9," Amesema Dkt Mang'enya.
Naye Makamu Mwenyewe wa Bodi CPA Felix Maagi amesema katika kutambua umuhimu wa ushirikishwaji wa kifedha katika ujenzi wa uchumi wa taifa Benki ya Azania imeanzisha Akaunti maalumu.
"Akaunti hizo zipo kwenye makundi malimbali kama makundi ya akinamama, vijana, wastaafu na sekta ya biashara hasa makampuni madogomadogo ambapo Benki inaziangalia sekta hizo kwa jicho la kipekee hasa kwa kuweka akiba katika kukuza biashara, " Amesema
0 Comments