Header Ads Widget

WANANCHI WA IRINGA WAKUMBUKUSHWA KUDUMISHA UTAMADUNI KWA KUKUZA UTALII WA UTAMADUNI

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA 

WANANCHI mkoani Iringa wametakiwa kudumisha na kuthamini utamaduni wao kama njia ya kuvutia watalii kutoka mataifa mbalimbali, hatua ambayo itachangia kukuza uchumi wa eneo hilo na kuboresha maisha yao binafsi. 


 Jimson Sanga mkurugenzi wa Makumbusho ya Mkoa wa Iringa aliyasema hayo wakati wa kongamano la Miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha .

Sanga alisema kuwa utalii wa utamaduni ni fursa muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwa kutumia mila, desturi, vyakula, na vinywaji vyao kuwavutia wageni. 

Kuwa hii inawapa nafasi ya kipekee ya kuingiza kipato kupitia shughuli zao za kila siku, na kuwaelimisha wageni kuhusu maisha yao ya kila siku.

"Utalii wa utamaduni unawapa wananchi thamani na kuwafanya waone kwamba wanaweza kuishi na wageni na kuwahusisha moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku. 

Badala ya wananchi kuona tu magari ya watalii yakipita kuelekea Ruaha National Park, wanapaswa kuelewa kwamba utalii unahusisha zaidi kuliko kuona wanyama pori pekee, ni namna ya kuishi na wageni pia," alisema Sanga.


Alitolea mfano wa Wamasai ambao wamekuwa wakitumia mila na desturi zao kama kivutio kikubwa cha utalii. Alisema kuwa Wamasai wamefaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na utamaduni wao kuvutia watalii, jambo linaloleta fedha nyingi kwa jamii yao.

"Nilienda Serengeti na nikaona Wamasai wakiwaonyesha wageni simba wanapowinda, jambo ambalo linawavutia sana watalii na kuwalipa fedha nyingi. 


Kwa hiyo, jamii za Iringa zinapaswa kufikiria njia za kutumia utamaduni wao kuvutia wageni," aliongeza Sanga.

Pia alitoa wito kwa taasisi zinazohusika na utalii nchini kuhakikisha zinatenga bajeti maalum kwa ajili ya kuhusisha moja kwa moja wananchi katika sekta ya utalii.

 Alisisitiza umuhimu wa kurejesha michezo ya asili, tiba za asili, na ujenzi wa nyumba za asili ili kuboresha utalii wa utamaduni katika eneo hilo.

MRADI WA REGROW NA MAFANIKIO YAKE KWA WANANCHI WA PEMBEZONI MWA HIFADHI YA RUAHA

Hata hivyo wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wameendelea kunufaika na misaada inayotolewa na Mradi wa Regrow kutokana na ushirikiano mzuri kati yao na hifadhi hiyo.

Michael Joseph, Msimamizi wa Mradi wa Regrow, alibainisha kuwa mradi huo, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, umeleta mafanikio makubwa katika kuboresha maisha ya wananchi.

Miongoni mwa misaada inayotolewa ni pamoja na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi, kuanzisha benki za kijamii, na kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo. Pia, Mradi wa Regrow umekuwa ukishirikiana na Rufiji Basin katika kutunza Mto Ruaha ili kuzuia uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.


 "Mradi wa Regrow umesaidia kutoa elimu kwa jamii, hasa kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi, na pia kuanzisha benki za kijamii ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanaozunguka hifadhi," alisema Joseph.

Mradi huo umeendelea kuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Iringa, na unatarajiwa kuchangia zaidi katika kuimarisha maisha ya wakazi wa eneo hilo kwa miaka ijayo.



KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA HIFADHI YA TAIFA YA RUAHA KITAHITIMISHA NA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII BALOZI DR PINDI CHANA TAREHE 7/10/2024

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI