Fadhili Abdallah,Kigoma
VIONGOZI wa dini na vyama vya siasa mkoani Kigoma wametoa kauli mbele ya viongozi wa serikali wakisema kuwa wako tayari kushirikiana na serikali kuufanya uchaguzi wa serikali za mitaa kuwa uhuru, wa haki na amani.
Viongozi hao wametoa kauli hiyo walipokuwa kwenye mkutano wa pamoj viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye aliyekuwa akitoa maelekezo ya sheria na taratibu za kufuatwa katika uchaguzi huo ili kuufanya uchaguzi kuwa wa amani unaozingatia sheria za uchaguzi nchini.
Mjumbe wa baraza la Mashekhe mkoa Kigoma (BAKWATA), Kapipi Baraka alisema kuwa mkutano huo umetoa mwanga mkubwa kwao kuelekea kwenye uchaguzi huo kwa kuwashirikisha na kujua taratibu mbalimbali za uchaguzi jambo ambalo halikuwa kufanyika hivyo wanaimani uchaguzi huu utakuwa huru, haki na amani.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jumuia ya Kikristo Tanzania (CCT) mkoa Kigoma, Mchungaji Melzedek Hozza alisema kuwa wao kama viongozi wa dini wako tayari kuunga mkono serikali kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru,amani na shirikishi ili kila mwenye kigezo aweze kuchagua na kuchaguliwa.
Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) mkoa Kigoma, Yassin Abdallah maarufu Mambo Bado alisema kuwa kwa mara ya kwanza serikali ya mkoa Kigoma imefungua milango kuelekea uchuguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu na wao kama vyama vya siasa wanaunga mkono kuhakikisha uchaguzi utakuwa na amani kila mwananchi aweze kushiriki kwa kadri anavyoona inafaa kwa nafasi aitakayo pia kutoa fursa kwa wananchi kuchagua kiongozi wanayempenda.
Akizungumza katika mkutano huo MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amesema kuwa masuala ya dini na ukabila siyo vigezo ambavyo vitazingatiwa katika kuwapata wagombea na wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambao mchakato wake umeanza.
Mkuu huyo wa mkoa aliwaambia viongozi hao kuwa sheria,kanuni na taratibu za uchaguzi ziko wazi hivyo aliwataka viongozi hao ambao wana makundi makubwa ya watu nyuma yao wakiwemo wagombea na wapiga kura kuzijua sheria, kanuni, taratibu na miongozi inayosimamia uchaguzi huo wa serikali za mitaa.
0 Comments