NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Mbeya vijijini Getruda Japhet Lengesela, ameeleza kukerwa na mfumo wa Serikali anaosema ni mbovu katika kuwaletea wananchi maendeleo na kwamba bado hali ya maisha na usalama wa wananchi ni mdogo.
Amesema wananchi wanaonekana kuwa na hofu kutokana na kughubikwa na matukio ya uhalifu hasa watu kutekwa ambapo amesema tatizo lipo kwenye uongozi kwa wananchi wanaowaongoza.
Getruda amesema hayo wakati wa mazungumzo yake na waandishi habari kuhusu mwenendo wa siasa za Tanzania na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa ambapo amesema kipindi cha kampeni na chaguzi Chama Cha Mapinduzi huendekeza chuki na fitina wakati siasa sio uadui.
Pamoja na hayo amesema Chama chake (CHADEMA) kimejipanga vilivyo kuhakikisha kinashiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji na kutaka atakayeshinda akatangazwe badala ya kuendekeza mfumo wa kupita bila kupingwa anaosema hautovumiliwa kwenye jimbo lake katika chaguzi zijazo.
Amesema CHADEMA haitavumilia kuona mazingira ya mwaka 2019/2020 yanajirudia kwenye chaguzi za mwaka huu na mwakani badala yake wananchi waachwe wachague viongozi wanaowataka.
"Angalizo, kipindi cha chaguzi Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikionyesha chuki, fitina na figisu mbalimbali na kutumia vyombo vya dola kupata ushindi jambo ambalo halitavumiliwa hivyo niviombe vyombo vya dola hasa Polisi acheni kuingilia masuala ya kisiasa", amesema kiongozi huyo.
Pamoja na hayo amehimiza wanachama na wananchi kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa kuhakikisha wanachagua viongozi bora kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani 2025.
0 Comments