Header Ads Widget

UTPC KUFANYA MKUTANO MKUU WA MWAKA MKOANI SINGIDA, YATOA NENO KUHUSU UCHAGUZI

 



Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA 


MUUNGANO wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) utafanya mkutano mkuu wa mwaka kuanzia kesho (Novemba 1, 2024) mkoani Singida ambao utafunguliwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.


Rais wa UTPC, Deogratius Nsokolo, akizungunza na waandishi wa habari leo (Oktoba 31, 2024) mjini Singida, amesema mkutano huo ambao ni wa kawaida wa kupitia shughuli ambazo zimefanywa mwaka uliopita na kuangazia shughuli ambazo zitafanyika kwa mwaka ujao.


"Mkutano Mkuu wa UTPC unashirikisha wajumbe watatu kutoka kila mkoa ambao ni Mwenyekiti wa Klabu, Katibu na Mweka Hazina,na utatanguliwa na Bodi ya Wakurugenzi ambao watakutana leo (Alhamisi) kwa ajili ya maandalizi ya mkutano mkuu," amesema Nsokolo.


Amesema mwaka huu wameamua kufanya Mkutano Mkuu mkoani Singida, lengo ni kusogeza karibu na wanahabari ili waweze kufahamu mazingira ambayo waandishi wa Singida wanafanya shughuli zao za kila siku na kuwapa fursa waandishi wote kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar kuweza kujifunza na kujua nini kinaendelea Singida.


Nsokolo amesema Novemba 2, 2024 ambayo itakuwa ni siku ya kimataifa ya kukomesha uharifu dhidi ya waandishi wa habari, siku hiyo kwa Tanzania itaadhimishwa katika Mkoa wa Singida na waandishi zaidi ya 100 ambao wanatoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.


"Hii ni siku kubwa kwa waandishi kwani tunakumbana na changamoto ambazo zinahatarisha kazi zetu lakini pia zinahatarisha maisha yetu," amesema Nsokolo.


Ameongeza kuwa jioni ya Novemba 2, 2024 UTPC itatoa tuzo za weledi kwa waandishi wa habari wa kike na wa kiume kutokana na kuandika habari ambazo zimeleta matokeo chanya katika maeneo yao ambazo zitatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego.


"Wito wangu siku mbili hizi tukiwa Singida tuzitafakari ni kwa namna gani tunasaidia kuleta maendeleo katika nchi hii ni kwa namna gani tunaandika habari ambazo watawala wanazipa nafasi kufanya mabadiliko ya kiuchumi,kijamii na kisiasa katika maeneo mbalimbali hatimaye kuleta nafuu kwa wananchi," amesema Nsokolo.


Nsokolo amesema ni habari tu ndizo ambazo zinaweza kuleta mabadiliko na hivyo UTPC ipo tayari kuongozana na waandishi ili kufikia malengo panapohitajika kwamujibu wa sheria na katiba ya nchi.


UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA NA UCHAGUZI MKUU


Rais wa UTPC, Nsokolo, akizungumzia kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemva 27, 2024 na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani, amewataka wanahabari kutimiza wajibu wao wa kuandika habari zitakazowafanya wananchi kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi bora watakaokuja kusaidia maendeleo yao.


"Uchaguzi ni zoezi moja kubwa sana kwani kupitia viongozi ndipo unaweza kupata kiongozi bora au wa hovyo,hivyo basi wanahabari tunapaswa kutimiza wajibu wetu wa kuwafanya wananchi waweze kuchagua viongozi bora ambao watakuja kusaidia maendeleo yao," amesema.


Nsokolo amesema UTPC inawajibika kutoa mafunzo kwa wanahabari katika kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaofanyika mwaka huu uchaguzi mkuu mwakani ili kuwajengea uwezo waandishi wa habari waweze kusaidia wananchi kuchaguzi viongozi wazuri.


"UTPC ambayo inaongoza klabu 28 za waandishi wa habari Tanzania Bara na Visiwani na inahudumia takribani waandishi 2000 kwa vyovyote jambo ambalo linahusiana na uchaguzi ni jambo kubwa sana ambalo linakwenda kuleta viongozi kwenye taifa letu ambao watakuja kusimamia maendeleo ya nchi hii," amesema.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, alisema suala la kuwajengea waandishi uwezo au ujuzi wa kuandika habari za uchaguzi zenye weledi ni suala ambalo limepewa kipaumbele na UTPC.


"Tunapompa mwananchi habari ndipo wanaweza kuchagua viongozi sahihi, hivyo kama taasisi tunalipa kipaumbele kikubwa suala la kuwapa mafunzo waandishi kwani tunaamini endapo waandishi hawatawapa wananchi habari sahihi hawatachagua viongozi ambao ni sahihi wa kuwaletea maendeleo," alisema.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI