Header Ads Widget

OPARESHENI YA SHIUMA YA MAMA SAMIA TUVUSHE 2025 IUNGWE MKONO NA MAKUNDI YOTE





katibu wa itikadi na uenezi CCM mkoa wa Iringa Joseph Ryata  (mwenye kofia) akizindua oparesheni ya Mama Tuvushe 2025 "kwa kuonesha Ti-sheti maalum iliyobeba ujumbe wa Mama Tuvushe 2025 kushoto kwake  ni Katibu mkuu wa SHIUMA Taifa Venatus Magayane na kulia kwake naibu katibu mkuu wa SHIUMA Taifa Joseph Mwanakijiji na viongozi wengine .picha na Matukio Daima media 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA 


"MAMA TUVUSHE 2025 " ni oparesheni yenye kumheshimisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan iliyobuniwa na kundi la wafanyabiashara Ndogo Ndogo Maarufu kama Machinga kupitia shirikisho lao la SHIUMA .

Kila kundi limekuwa na  mipango yake na hata matumaini kwa kiongozi awaye yeyote.

Katika kampeni ya urais ya mwaka 2025 kundi la SHIUMA linakuja na Kauli mbinu yake ya  "mama Tuvushe 2025," ikilenga kuendeleza mafanikio na kuimarisha maendeleo ya taifa kwa ajili ya mustakabali wa Watanzania wote. 

Hii ni sehemu ya ahsante ya Machinga kwa Rais Samia ambae  amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa Tanzania inasonga mbele kwa kasi katika nyanja zote za kijamii, kisiasa, na kiuchumi.

Kampeni hii inajikita katika kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana wakati wa uongozi wake, huku ikilenga  kuleta fursa mpya zaidi kwa wananchi.


Rais Samia ameweza kuimarisha sekta ya miundombinu kwa kujenga na kukarabati barabara, madaraja, na viwanja vya ndege, hatua inayochochea uchumi kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu. 

Mradi mkubwa wa reli ya kisasa (SGR) na miradi ya umeme kama Bwawa la Nyerere ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya awamu yake, na katika kampeni ya Tuvushe 2025, anatarajia kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa ufanisi.

Katika sekta ya afya, Rais Samia ameongeza bajeti ya afya na kuimarisha huduma za msingi za afya vijijini na mijini kwa kujenga zahanati na vituo vya afya.


 Kampeni yake imelenga kuendelea kuboresha huduma za afya, kwa kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana na wananchi wanapata huduma bora za matibabu.

Pamoja na hayo, Rais Samia amejitolea kuimarisha elimu, kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu ya bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Katika Tuvushe 2025, anaahidi kuongeza juhudi za kuboresha mazingira ya shule, kutoa mafunzo kwa walimu, na kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kufundishia.


Kampeni ya Mama  Tuvushe 2025 inalenga pia kupongeza na kumtia nguvu Rais katika kuongeza ajira kwa vijana kupitia programu za kukuza ujuzi, kuanzisha viwanda, na kuboresha mazingira ya biashara. 

Rais Samia amejikita katika kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, hivyo kuzalisha fursa nyingi za ajira. 


Kwa kuzingatia uchumi wa kidijitali, anatarajia kuongeza programu za mafunzo ya teknolojia ili vijana waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa.

Katika utawala wake, Rais Samia amejitahidi kulinda haki za kidemokrasia, kujenga misingi ya utawala bora, na kukuza uhuru wa vyombo vya habari. 

Kupitia kampeni ya Tuvushe 2025, anawahakikishia Watanzania kuwa ataendelea kuimarisha demokrasia, haki za binadamu, na usawa wa kijinsia kwa kuhakikisha kuwa sauti za kila raia zinasikika na kuheshimiwa.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na mamia ya Wamachinga kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa, ajenda kuu ilikuwa kuimarisha umoja wao ili kupambana na changamoto zinazowakabili katika biashara zao. 

Katika mkutano  wa kihistoria waachinga Iringa na uongozi wa SHIUMA Taifa mkutano uliohudhuriwa na viongozi wa Chama Cha mapinduzi (CCM)wawakilishi wa benki, na viongozi wa taasisi mbalimbali, ambao waliwapa Wamachinga mwelekeo wa namna bora ya kufanya biashara kwa mafanikio zaidi. 

Kauli ya mshikamano na kuachana na migogoro ya ndani ilikuwa moja ya mada muhimu zilizojadiliwa.



Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Joseph Nzala Ryata, alifungua kikao hicho kwa hotuba iliyoeleza umuhimu wa umoja na ushirikiano miongoni mwa Wamachinga. 

Alisema, “Migogoro isiyo na tija haileti maendeleo. Tunatakiwa kuacha tabia za kugombana na kuwekeza kwenye mshikamano na ushirikiano. Umoja wenu ni nguzo muhimu kwa mafanikio yenu ya kibiashara.”

Ryata alilaani vikali vitendo vya matumizi ya nguvu kuwafukuza Wamachinga kutoka maeneo yasiyo rasmi ya kibiashara, akisema kuwa vitendo hivyo vinavunja amani na ushirikiano katika jamii.

 Aliwataka viongozi wa serikali na vyombo vya dola kutumia njia za kidiplomasia na majadiliano badala ya nguvu ili kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto hiyo.

Kwa kuangalia hali ya soko la dunia, Ryata alisisitiza kuwa biashara ya nguo ni moja ya fursa muhimu kwa Wamachinga.

 Alisema, “Watu wanapenda mitindo ya kisasa. 

Ni muhimu kujikita zaidi kwenye bidhaa zinazofikia mahitaji ya wateja wa sasa. Mabadiliko ya mitindo na mahitaji ya wateja yanapaswa kuwa kipaumbele kwa wafanyabiashara wote.”


Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Iringa Mjini, Godfrey Francis, alisisitiza juu ya umuhimu wa umoja na mshikamano kati ya Wamachinga.

 “Hatuwezi kufanikiwa kama tunafanya kazi kwa migawanyiko. Umoja wenu ndiyo utakaowezesha biashara zenu kufanikiwa,Tunapofanya kazi kwa pamoja, tunakuwa na nguvu kubwa zaidi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali.”

Francis aliwaasa Wamachinga kujiepusha na migogoro ya ndani ambayo imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo yao ya kibiashara. 

Alisema kwamba, migogoro inapoendelea, inaleta mgawanyiko na kudhoofisha uwezo wao wa kupigania haki zao na kushirikiana kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.

Alisema pia kuwa ni muhimu kuzingatia nidhamu katika biashara. “Nidhamu ni nguzo muhimu sana katika mafanikio ya biashara. Bila nidhamu, hata kama mnapata fursa nzuri, hamuwezi kuzitumia ipasavyo,” aliongeza.


Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Mkwawa, Stanlausy Mwendi, alisisitiza kuwa benki yake imejipanga kuwawezesha Wamachinga kupata mikopo kwa masharti nafuu ili kuboresha mitaji yao.

 Alisema, “CRDB ipo tayari kufanya kazi na Wamachinga. Tunatoa mikopo nafuu na huduma za kifedha ambazo zinaweza kuwasaidia kufanikisha malengo yenu ya biashara  ni muhimu muunde vikundi vidogo vidogo ili kupata mikopo kwa urahisi zaidi.”

Mwendi alieleza kuwa, kujipanga katika vikundi ni njia bora kwa Wamachinga kupata dhamana ya mikopo na hivyo kuongeza uwezo wa kupata mitaji mikubwa zaidi.

 Alisema kuwa njia hii si tu itaongeza upatikanaji wa mikopo, bali pia itawajengea uwezo wa kusimamia mikopo na kurejesha kwa wakati.

Pamoja na kutoa mikopo, Mwendi alihimiza matumizi ya teknolojia za kisasa katika uendeshaji wa biashara zao. 

Alisema, “Leo hii dunia imebadilika. Malipo ya kidijitali yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku. 

Ni muhimu mfanye biashara zenu kwa kutumia njia hizi za kisasa ili kuendana na mahitaji ya wateja wenu.”

Yahaya Mpelembwa  Mwenyekiti  wa Wamachinga  Smart Mkoa wa Iringa, alisisitiza juu ya umuhimu wa kushirikiana na makampuni na taasisi mbalimbali ili kupata fursa zaidi. 

Alitaja makampuni kama Vodacom na CRDB kama mifano ya mashirika ambayo yanaweza kutoa msaada wa kifedha na vifaa kwa Wamachinga ili kuboresha biashara zao.

Mpelembwa alieleza kwamba, “Tunapoanzisha ushirikiano na taasisi kama hizi, tunapata nafasi ya kukuza biashara zetu.

 Tunapaswa kutumia fursa hizi kwa umakini na kuhakikisha kuwa kila fursa inayojitokeza inatumiwa vizuri kwa maendeleo ya kila mmoja wetu.”

Aliwaasa Wamachinga kuanza upya kwa nguvu na ari mpya.

 Alisema, “Huu ni wakati wa kuacha migogoro na kuangalia fursa zinazotuzunguka. Dunia inabadilika na fursa ni nyingi. 

Tunatakiwa kutumia kila fursa inavyotokea, na hii itatuhakikishia maendeleo yetu.”


Katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA), Venatus Magayane, alitangaza rasmi kuwa wamefikia makubaliano na kufuta kesi iliyokuwepo dhidi ya Katibu Msaidizi wa Shirikisho hilo, Joseph Mwanakijiji. 

Kesi hiyo, ambayo ilikuwa imefunguliwa mwaka 2023, ilikuwa ikihusisha mgogoro wa kiuongozi ndani ya umoja wa Wamachinga, hali ambayo ilizua migawanyiko na kuzorotesha juhudi za maendeleo.

Magayane alisema kuwa makubaliano hayo yamefikiwa baada ya majadiliano ya kina, na kwamba sasa ni wakati wa umoja na mshikamano.

 Alisema, “Migogoro hii ilikuwa inatuchelewesha. Sasa tumeamua kuanza upya kwa pamoja, na hii ni ishara kuwa tunatakiwa kuweka mbele maslahi ya pamoja badala ya migogoro isiyo na tija.”

Uamuzi huo wa kumaliza migogoro na kuanza upya uliungwa mkono na Wamachinga waliokuwa wakihudhuria kikao hicho. 

Walieleza matumaini yao kwamba, umoja huo mpya utasaidia kufanikisha biashara zao na kuboresha maisha yao. 

Wamachinga wengi walionyesha nia yao ya kufanya kazi kwa pamoja ili kupata mafanikio ya haraka na kudumu.

Huku Naibu katibu mkuu Taifa wa SHIUMA Joseph Mwanakijiji alisema kuwa kumalizika kwa tofauti zao ni Mwanzo mpya wa kujenga SHIUMA mkoa wa Iringa.

Mkutano  Wamachinga Iringa umekuwa na mafanikio makubwa na Moja kati ya mkakati Wao ni kuahidi kushirikiana kwa dhati na kuanza upya, wakiwa na malengo ya kuboresha biashara zao na kuongeza kipato.

 Viongozi wa Chama tawala na taasisi mbalimbali walitoa ahadi ya kuendelea kushirikiana nao na kuwapa msaada wa kifedha, kiushauri, na kielimu ili kufanikisha maendeleo yao.

Wamachinga walitoka kwenye mkutano huo wakiwa na matumaini makubwa, wakiamini kuwa juhudi za pamoja na umoja wao zitaleta matokeo chanya katika biashara zao.

 Pia, walikubaliana kwamba nidhamu, uwazi, na uaminifu vitakuwa misingi muhimu katika safari yao ya kuendeleza biashara na kujiletea mafanikio.

Ni wazi mkutano huo ulitoa mwanga wa matumaini kwa Wamachinga wa Iringa.

 Umoja wao mpya umejikita katika kuimarisha ushirikiano, kutumia fursa za kifedha na kibiashara zinazojitokeza, na kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kufikia malengo yao ya kibiashara. 

Wamachinga wa Iringa wameweka nia thabiti ya kuachana na migogoro na kujikita zaidi kwenye kujenga mazingira bora ya biashara kwa ajili ya maendeleo yao na jamii inayowazunguka.

Ifahamike kuwa mkoa wa Iringa hadi sasa bado haujawa mwanachama halisi wa SHIUMA kwani SHIUMA Taifa inaundwa  Vyama 10 Pekee ambavyo ni KAWASO,GAWASO,KIBINDU,MOWASO,KAGERA,PWANI,MBEYA ,DODOMA ,GEITA NA RUKWA .

Hivyo kupitia mkutano huu na kumalizika kwa tofauti hizi ni safari mpya imeanza mkoa kujiunga na SHIUMA kupitia Vyama kama Machinga Smart ama Machinga Network Iringa.

Mwisho 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI