Header Ads Widget

DC MWANSASU: WATAKAOSHIRIKI KUUNDA VIKUNDI HEWA VYA MIKOPO YA 10% KUKUTANA NA MKONO WA SHERIA.

Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE

Kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1.3 kimetengwa kwa ajili ya utoaji Mikopo ya vikundi vya wanawake,Vijana na wenye Ulemavu katika Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe kupitia mapato ya ndani na kwamba fedha hizo zigawanywe kwa usawa katika Tarafa zote tatu za wilaya.

Akitangaza Marejeo ya mikopo hiyo iliyositishwa tangu mwaka 2023 Mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe Zakaria Mwansasu amesema hataki kusikia fedha hizo zimepelekwa maeneo machache kwa upendeleo na kwamba zinapaswa zikalete maendeleo kwa usawa.

Katika mafunzo kwa wataalamu ngazi ya Halmashauri hiyo Mwansasu amewaonya wataalamu watakaojihusisha na uundaji vikundi hewa na kwamba fedha hizo zitawatokea puani.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Wanging'ombe Nicephorus Mgaya amekiri kupokea maelekezo ya mkuu wa wilaya na kuahidi kufanyia kazi kikamilifu katika utoaji wa mokopo hiyo.



Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri hiyo Bwana Mkali Japhet Kubebeka amesema miongoni mwa kanuni zilizopo katika utoaji mikopo hiyo ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wanakikundi kitakachoshindwa kufanya marejesho kwa mujibu wa muda uliotolewa huku udanganyifu ukionywa vikali.

Rosemary Kapoma ni Mratibu wa mikopo hiyo ambaye Amesema wanufaika wa Mikopo kwa upande wa vijana kwa sasa ni kuanzia miaka 18 hadi 45 tofauti na hapo awali vijana walikuwa wanakomea miaka 35 huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiingizwa kwenye kamati ya uhakiki na ufuatiliaji.

Kwa upande wao wananchi wa Wilaya ya Wanging'ombe akiwemo Peter Lupenza na Victor Mdzovela wamekiri kuwa mikopo hiyo ilikuwa na tija kubwa katika uchumi na maisha yao hivyo kurejea kwake itawasaidia kuboresha maisha yao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI