Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amewahimiza wanawake mkoani hapa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 na uchaguzi mkuu wa mwakani 2025 ili waweze kuwa na nafasi ya kushiriki katika ngazi za maamuzi.
Amesema hayo leo (Oktoba 9,2024) wakati akifungua kongamano la wanawake na uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 ambalo linawashirikisha wanawake kutoka wilaya zote za mkoa huu lengo likiwa ni kuwahamasisha kujitokeza kushiriki uchaguzi mwaka huu na mwakani.
"Nitumie nafasi hii kuwakumbusha kwamba 27 Novemba, 2024 ni siku ya uchaguzi wa Viongozi wetu wa Serikali za Mitaa (Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji) nchi nzima, Kaulimbiu ya uchaguzi huu inasema “Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo ya Taifa letu, maandalizi yote ya kufanikisha uchaguzi huu yamekamilika kwa kuanza na zoezi la uandikishaji wa wapiga kura lililofanyika kuanzia tarehe 25 Septemba, 2024 hadi tarehe 01 Oktoba, 2024,"amesema Dendego.
Amesema kampeni za uchaguzi zitaanza rasmi 20 hadi 26 Novemba 2024 na kuviomba vyama vyote vya siasa vitakavyoweka wagombea kufanya kampeni za kistaarabu kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Amesema Mkoa wa Singida kwa mujibu wa Sensa ya Watu na makazi ya mwaka 2022 unakadiriwa kuwa na jumla ya Watu 2,008,058, kati ya hao wanawake ni 1,012,355 sawa na asilikia 51 na wanaume ni 995,703 sawa na asilimia 49.
Amesema pamoja na mkoa kuwa na idadi kubwa ya wanawake lakini wenyeviti wanawake ni 96 tu, mitaa ipo 53 wenyeviti Wanawake wapo 03 tu na jumla ya Wanawake katika nafasi ya ujumbe wa Serikali katika ngazi zote wapo 3,125. Aidha, katika nafasi ya Udiwani kati ya Kata 136 za Mkoa, Madiwani Wanawake wapo 04 tu wa kuchaguliwa.
"Takwimu hizi haziridhishi, niwaombe wanawake wenzangu kwa kuanza na uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa twendeni tukapindue meza, tujitokeze kwa wingi kugombea nafasi zote kwani Sifa tunazo, uwezo tunao, vipawa na maarifa ya uongozi tunayo, wanawake ni Jeshi kubwa tukiamua tunaweza," amesema Dendego.
Aidha, Dendego amewataka wanawake kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kutoa malezi bora ili kujenga familia na jamii imara yenye hofu ya Mungu, yenye maadili mema yenye kufuata misingi ya maisha inayokubalika katika mila na desturi zetu.
"Napenda niwakumbushe kuwa malezi ya mwanamke hayaishii kwa watoto tu bali hata kwa baba wa watoto wetu. Yupo kiongozi wa dini na mfanyabiashara maarufu raia wa Marekani Bw.Russel Ballard aliwahi kusema, nanukuu… THERE IS NO ROLE IN LIFE MORE ESSENTIAL AND MORE ETERNAL THAN THAT OF MOTHERHOOD akimaanisha kwamba katika maisha hakuna jukumu muhimu na la milele kuzidi malezi ya mama," amesema Dendego.
Amesema wanawake ni lazima wasimame imara katika malezi ya watoto na kutotoa nafasi kwa kuwaacha walelewe na mitandao ya kijamii kama facebook, Instagram, Twitter, WhatsApp) ambayo isipotumika kwa usahihi ni chanzo kikubwa cha kumomonyoka kwa maadili na ni lango la mitindo ya kigeni ya maisha ambayo yapo kinyume na imani, mila na desturi zetu.
Ameongeza kuwa wanawake wana haki sawa na wanaume katika kufanya kazi na kumiliki mali hivyo wasiwe wanyonge au kusubiri kuletewa kwani zipo fursa mbalimbali zinatolewa na Serikali na hata katika taasisi zisizo za Kiserikali kwa ajili ya wanawake kuinuka kiuchumi, ipo mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu inayotolewa katika halmashauri.
"Chini ya Uongozi wa Rais wetu mpendwa, jemedari wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan mama wa upendo fursa kubwa za kiuchumi zimeendelea kufunguka. Kupitia sera ya Taifa ya uwezeshaji mheshimiwa Rais wetu ametuletea fursa nyingine ya programu ya
“IMARISHA UCHUMI NA SAMIA” (IMASA). Programu hii itahusika kuwawezesha Kiuchumi Wanawake,Vijana na Watu wenye mahitaji maalumu ambao wamerasimishwa iwe ni kundi au mtu mmoja mmoja katika mikoa yote na Singida tukiwemo," amesema Dendego.
Naye Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Anne Makinda,amewataka wanawake katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wajiandikishe,wagombee nafasi za uongozi na kwenda kupiga wasipofanya hivyo itakuwa imekula kwao kwani ushindi ni hesabu.
Makinda ambaye pia ni Kamisaa wa Sensa, amesema wanawake wanatakiwa kufanya maajabu katika chaguzi hizo kwa kuhakikisha rais anakuwa mwanamke,wenyeviti wa vitongoji,vijiji na mitaa nao wanakuwa wanawake hadi dunia ishangae.
"Tujiandikishe na tukapige kura tusipopiga kura imekula kwetu kwani ushindi ni hesabu,maana mama (rais) anasifika sana mara asante kwa maji,asante kwa barabara basi nyie mnafikiri mama anapita asubuhi,hapana ni hesabu hata viongozi wetu wa mitaa,vitongoni ni hesabu," alisema.
Makinda amesema wanawake wanapendaga kudhalau vitu ningi lakini katika suala la uchaguzi wanawake wawapeleke watoto kujiandikisha na kupiga kura ili kupata viongozi wengi wanawake kwani uwekezaji katika nchi unataka demokrasia.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa,amesema idadi ya watu Tanzania imeongezeka sasa na kufikia milioni 65 mwaka huu kutoka milioni 61.7waliotangazwa wakati wa kutoa matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
"Nchi yetu imebarikiwa sana,tulikuwa na sensa ya watu na makazi 2022 sasa hivi nchi yetu ina watu milioni 65 kwa makadirio yaliyopo 2024 na kwa Mkoa wa Singida wamefikia watu milioni 2.1 kutoka watu 2,008,000 waliokuwepo 2022," alisema.
Dk.Chuwa amesema kwa kuwa idadi ya wanake bado inaendelea kuwa kuvwa hivyo wajitokeze kujiandikisha na kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa bila kufanya masihala.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatuma Mganga, amesema kongamano hili ni kwa ajili ya kuhamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Amesema uwakilishi wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi katika mkoa ww Singida ni mdogo sana mfano katika vitongoji 2000 vilivyopo mkoani Singida uwakilishi wa wanawake kwenye uongozi ni asilimia 4 tu.
Dk.Mganga amesema katika vijiji 441 vilivyopo Mkoa wa Singida ni wanawake watano tu ndo walipata nafasi ya uongozi kuwa wenyeviti wa vijiji ambao ni sawa na asilimia moja tu wakati katika kata 136 ni kata nne tu ndo waliokwenda kuchukua kata.
"Katika Manispaa ya Singida kuna mitaa 53 lakini wanawake waliodhubutu kuchukua fomu na kushinda ni watatu tu wakati katika nafasi ya ujumbe kati ya nafasi 11,000 za wajumbe wa serikali za mitaa wanawake 3,125 ndo wajumbe wa serikali za mitaa," alisema.
Dk.Mganga amesema kutoka na uwakilishi mdogo wa wanawake katika uongozi serikali ya Mkoa wa Singida imeona haiwezi kujamazia suala hili hivyo imeakua kuandaa kongamano ili kuwapa uelewa na ujasiri wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
0 Comments