-Naye ajaribu kujiua bila mafanikio, wananchi wazua gari la wagonjwa lisimuhishe hospitali.
-Akaa saa 10 utumbo ukining’inia nje.
Na Moses Ng’wat, Songwe.
MKAZI wa kijiji cha Kapeta, kata ya Ikinga, Wilayani Ileje, Mkoani Songwe, Wema Ndile (29) ameuawa kwa kuchomwa na kisu kitovuni na shingoni na mtalaka wake aliyetengana naye kwa kipindi cha miezi mitano.
Mtuhumiwa huyo, Ally Mwakilembe (42) ambaye kwa sasa amelazwa katika moja ya Hospitali Wilayani humo, chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi baada naye kujaribu kujiua kwa kujichoma na kisu tumboni baada ya kutekeleza mauaji hayo.
Taarifa za uhakika zilizopatikana kutoka eneo la tukio na baadae kutbibitishwa na Mtendaji wa Kijiji cha Kapeta, Octatus Wangu, zinadai kuwa, mwanaume huyo alitekeleza mauaji ya mtalaka wake huyo baada ya kumvamia usiku wakati amelala katika chumba alichokuwa amepanga (Geto) Kijijini hapo.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wetu, Mtendaji wa Kijiji hicho, Wangu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba lilitokea majira ya saa nane usiku ya Oktoba 16, 2024.
Wangu amedai kuwa kabla ya mauaji hayo kutokea, mtuhumiwa alikuwa katika harakati za kumshawishi mtalaka wake amrudie baada ya kutengana kwa miezi mitano.
Alisema kuwa, ndoa ya wawili hao ilidumu kwa kipindi cha miaka 10 na kufanikiwa kupata watoto wawili, lakini baadae mwanamke (marehemu) aliamua kutengana na mumewe akimtuhumu kuzidisha ulevi na kusahau majukumu ya familia.
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida gari la wagonjwa limenurika kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali wakipinga kitendo cha kutaka kumuwahisha majeruhi hospitali wakitaka naye afie hapo.
Hali hiyo, ilisababisha majeruhi huyo kukaa zaidi ya saa 10, huku utumbo wake ukiwa nje akisubiri msaada kutoka jeshi la polisi wa kituo kikuu cha Wilaya ya Ileje, kilichopo umbali wa zaidi ya 100 ambapo baada ya kufika eneo la tukio walilazimika kuwatanya wananchi hao wenye hasira na kisha kumchukua majeruhi huyo.
Jitihada za kumtafuta Kamanda wa polisi Mkoa wa Polisi Songwe, Agostino Senga, hazikufanikiwa kwa kile kilichoelezwa kuwa yuko nje ya ofisi n hata simu zake zote hazikuweza kupatikana.
Mwisho.
0 Comments