MBUNGE WA MBEA VIJIJINI, ORAN NJEZA
NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza amewahimiza wananchi wake kujitokeza kwa wingi kuanzia Oktoba 11-20, 2024 kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili kushiriki kuchagua viongozi wanaowataka wa mitaa, vitongoji na vijiji.
Mbunge Njeza amesema hayo wakati akizungumza na kituo hiki kuhusu maandalizi ya uchaguzi na namna alivyohamasisha wananchi wake jimboni kuhakikisha wanajitokeza kujiandikisha.
"Wewe mwenyewe umeona hata leo nimetoka kwenye mkutano mkubwa wa hadhara ambapo nimehimiza wananchi kujitokeza kujiandikisha na nimekuwa nikihamasisha kwa vile ni muhimu sana", amesema Njeza na kuongeza;
"Ni imani yangu Mheshimiwa Rais (Dkt. Samia Suluhu Hassan) atakuwa raia namba moja kujiandikisha Dodoma kwahiyo na mimi kama Mbunge wake nipo tayari kuungana na viongozi wangu Mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya ya Mbeya na wananchi wangu jimboni kuhakikisha najiandikisha na kila mwananchi ajiandikishe kuanzia tarehe 11 Oktoba kwa ajili ya uchaguzi Novemba 27, 2024", ameeleza Mbunge Oran Njeza wa Mbeya vijijini.
Kwa upande wake mwenyekiti wa madereva wa bodaboda mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi David Mwazyunga, amewataka madereva katika vituo vyake vyote na Mbeya vijijini kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kujiandikisha huku wakihimiza pia familia zao ili kutimiza haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka kwa maendeleo yao.
Tausi Mwanshala ni mwananchi wa Mbalizi wilayani Mbeya, anasema amejiandaa vizuri kushiriki uchaguzi huo wa Serikali za mitaa.
"Binafsi nimejindaa vizuri kujiandikisha na niwaombe wananchi wenzangu tujitokeze kwenda kujiandikisha kwasababu ni haki yetu tukichagua viongozi tunaowataka tutakuwa na mamlaka nao na vile vitambulisho vya kadi havitumiki kwenye uchaguzi huu ila vitatumika 2025 kwahiyo saa hizi mpango ni kujiandikisha kwenye daftari la mkazi la mpiga kura", ameeleza mwananchi huyo mkazi wa Mbalizi Mbeya.
Zoezi la uandikishaji wapiga kura linatarajiwa kuanza Oktoba 11 hadi Oktoba 20 mwaka huu 2024 kwa ajili ya wananchi kushiriki haki yao kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka wa mitaa, vitongoji na vijiji kwenye uchaguzi huo mnamo Novemba 27, 2024.
0 Comments