-Wadau waungana na TFS kulinda ukanda wa pwani, wahamasisha wananchi kushiriki uhifadhi
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
DAR ES SALAAM: Wadau mbalimbali wa mazingira kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wamepanda zaidi ya miche 5,000 ya mikoko katika fukwe za Bahari ya Hindi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya ukanda wa pwani.
Zoezi hilo linalenga kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Denis Mwangama, aliwataka wananchi kufika katika ofisi za TFS ili kupata miche ya miti kwa ajili ya kupanda katika maeneo yao.
Alisema upandaji miti ni moja ya njia muhimu za kulinda mazingira, hususan katika maeneo ya pwani ambayo yanakabiliwa na changamoto za mmomonyoko wa ardhi na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari.
Mwangama alibainisha kuwa TFS imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo taasisi za Serikali na sekta binafsi, katika kuendesha kampeni za upandaji miti kote nchini.
Aliongeza kuwa ushirikiano huo umewezesha kufikiwa kwa mafanikio makubwa katika kuongeza uoto wa asili na kulinda rasilimali za misitu.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kunduchi, Marko Orio, alisifu juhudi hizo na kusema ni mfano bora wa kuigwa katika jamii.
Alisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya muda mrefu katika uhifadhi wa mazingira.
Orio alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuendelea kujitokeza kwa wingi katika shughuli za upandaji miti ili kulinda fukwe na mazingira kwa ujumla.











0 Comments