Na WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameshiriki katika mahafali ya 37 ya wanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Mlama iliyopo kata ya Kibosho magharibi kama Mgeni Rasmi.
Mbunge alifika shuleni hapo na kupokelewa na mkuu wa Shule Mwalimu Hugo Massawe, waalimu, viongozi wa serikali na mamia ya wananchi.
Baada ya mapokezi, Mbunge aliongozana na Mwalimu Mkuu kuona maonyesho ya taaluma kutoka kwa wanafunzi katika masomo ya biolojia, kemia na fizikia ambapo alifurahishwa na uelewa mkubwa aliouona kwa wanafuzi hao, na aliwazawadia washiriki wote.
Katika mahafali hayo Wahitimu na Mwalimu Mkuu walitoa risala zao mbele ya mgeni rasmi ambazo kwa ujumla zilieleza mafanikio na changamoto zinazoikabili Sekondari ya Mlama.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule Mwalimu Hugo Massawe alisema kuwa yeye na timu yake wameweka utaratibu wa kuwa karibu na wazazi na kila mwanafunzi ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wanafunzi wao.
Aidha aliwapongeza Walimu wake kwa jitihada kubwa ya kuwafundisha Wanafunzi, jambo ambalo limeifanya shule yao kuwa kimbilio la wazazi wenye kiu ya kuwapa elimu bora watoto wao.
Katika risala zote mbili, Changamoto zilizotajwa na wanafunzi pamoja na mkuu wa shule ilikuwa ni pamoja na Wazazi kuchelewa kulipa ada, Ukosefu wa Ukumbi wa shule, Ukosefu wa gari dogo la kusafirisha wanafuzi, ukosefu wa maabara ya fizikia, upungufu wa mipira na jezi.
Akiongea katika hadhara hiyo, Mbunge Ndakidemi alimpongeza Mwenyekiti wa Bodi na uongozi wa shule kwa usimamizi mzuri, jambo lililosababisha shule kuwa na maendeleo mazuri ya kitaaluma.
Aliwapongeza walimu kwa jitihada zao za kuwasaidia wanafunzi kwani Shule ya Mlama hufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha pili na nne.
Mbunge Ndakidemi aliwapongeza wazazi kwa kuwapeleka watoto kusoma katika Sekondari ya Mlama kwani wanapata elimu nzuri na malezi bora na kuwaomba waendelee kuwasaidia watoto wao na kushirikiana na walimu ikiwemo kulipa ada kwa wakati.
Ndakidemi aliwaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kushirikiana na bodi na uongozi wa shule ili kutatua changamoto zinazoikabili Sekondari ya Mlama.
Mbunge alihitimisha risala yake kwa kuwapongeza wahitimu, na kuwashukuru wazazi kwa jinsi walivyosaidia watoto wao kufikia mafanikio yao na kutoa mchango wake wa fedha taslimu kusaidia ukamilishaji wa maabara na vifaa vya michezo (jezi na mpira) kama alivyoombwa katika risali na kugawa vyeti vya kuhitimu kwa wanafunzi 38 na zawadi mbalimbali.
Mwisho
0 Comments