Header Ads Widget

MBUNGE WA JIMBO LA MOSHI VIJIJINI PROFESA PATRICK NDAKIDEMI AFANYA ZIARA YA KIKAZI KATA YA URU SHIMBWE.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI. 


MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amewatembelea wananchi wa Kata ya Uru Shimbwe ambapo aliongozana na Andrew Mwandu Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Diwani wa Kata ya Uru Shimbwe, Bertin Mkami, mwakilishi wa Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, pamoja na wataalamu kutoka TANESCO.


Katika ziara hiyo, Mbunge alimtembelea na kumsalimu Paroko wa Parokia ya Shimbwe Padri Joseph Mrina na kukagua ujenzi wa Choo cha Parokia na kuahidi kuchangia ujenzi unaoendelea wa choo hicho.



Katika kikao cha ndani, Mbunge alikutana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wa Kata ya Uru Shimbwe, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji na Mabalozi na badae kufanya mkutano wa hadhara katika Ofisi ya Kijiji  cha Shimbwe Chini ambapo aliwaeleza wananchi miradi ambayo Serikali imepeleka Uru Shimbwe kwa kipindi  cha miaka minne. 


Mbunge aliwaeleza wananchi kuwa mpaka kufikia mwisho wa mwezi wa sita 2024, Kata ya Uru Shimbwe ilipokea miradi ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Bilion 1,098,293,464.00.

 


Katika mkutano huo wa hadhara, Mbunge aliwahamasisha wananchi wajiandikishe na washiriki kikamilifu kwenye kuchagua  viongozi makini wa Serikali za mitaa, uchaguzi utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu.


Vilevile, alihamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa bima wa afya (NHIF) ambapo aliwaambia kuwa wakijiunga na NHIF  kadi ya bima itatumika kulipia gharama za matibabu katika zahanati, vituo vya afya na  hospitali zenye mikataba na NHIF. 



Aliwaambia kuwa wasipojiunga na bima ya afya, gharama za matibabu zinaweza kuwa kubwa sana kwa baadhi ya magonjwa. 

 

Katika mkutano wa ndani na ule wa hadhara,  wananchi waliibua kero mbalimbali ambapo suala la ujenzi wa barabara ya Mamboleo - Shimbwe Juu kwa kiwango cha Lami yenye urefu wa KM 13  ilikuwa ni kero iliyotawala.



Wananchi walisema kwamba barabara hiyo ilikuwa ni ahadi za Marais Jakaya Mrisho Kikwete na John Pombe Magufuli na kumwomba Mbunge afuatilie swala hili Serikalini. 


Kero ingine iliyoibuliwa na wananchi ni tatizo la kutokuunganishiwa umeme katika maeneo mbalimbali na kuomba kujumuishwa katika fursa ya kupatiwa umeme kupitia mradi wa REA.



Mwananchi mmoja alilalamika kuwa gharama za kutibiwa (hasa kwa wanawake wanaojifungua kwa upasuaji) ziko juu sana, jambo linalowafanya wananchi wa kawaida kushindwa kumudu hizo gharama.


Kwenye sekta ya kilimo, wananchi waliomba nguvu ielekezwe kwenye kukarabati  mifereji ya asili ili iwasaidie kwenye kuongeza tija kwenye kilimo cha kahawa na migomba vilevile waliiomba serikali ifanye udhibiti wa mbegu bora za mahindi, kwani kuna mbegu feki mitaani. 



Mbunge walishirikiana na Diwani na wataalamu na kujibu kero zote na zile kero ambazo hazikuwa na majibu walizichukua na kuwahakikishia wananchi kuwa watazipeleka kwenye mamlaka husika. 


Akizungumza kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya, Kaimu Katibu wa CCM  wilaya,  Andrew Mwandu alimshukuru Mbunge na Diwani  kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaletea wananchi wa Uru Shimbwe miradi mingi ya maendeleo.  



Aliwashauri Wana Shimbwe waendelee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge Ndakidemi na Diwani Mkami kwani kazi walizofanya ni kubwa na zenye tija na Wananchi kwa ujumla wanasonga mbele kimaendeleo.


Aliwashauri wananchi wajiandikishe na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2024. 


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI