NA WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amekutana na kufanya kikao na viongozi wa Dini kutoka madhehebu mbalimbali yanayotoa huduma Wilayani humo kwa lengo la kuwaeleza juu ya suala zima la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu 2024.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwapatia ratiba yenye matukio yote muhimu kuelekea siku hiyo na kuwasisitiza viongozi hao kuhakikisha ratiba hizo wanazisoma kwa waumini wao wakati wa ibada ili waumini wawe na uelewa kuhusu Uchaguzi, lakini kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua au kuchaguliwa.
Aidha pamoja na suala hilo, viongozi hao wa Dini walielezwa mambo mbalimbali yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya utawala wake.
Mkuu huyo wa wilaya amesema katika kipindi hicho Wilaya ya Same imepokea zaidi ya shilingi bilioni 58 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta zote ambapo amesisitiza pia Serikali ya Wilaya itaendelea kusimamia kwa karibu fedha zote zinazoletwa kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa kwa kuzingatia ubora wa miradi ili iendane na thamani ya fedha kuwezesha kuwa na manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wao viongozi hao wa Dini wamempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa aliyoyafanya Wilayani humo kwa kuleta fedha nyingi za maendeleo ambazo zimesaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati na kuboresha huduma za kijamii.
Pia wamepongeza utaratibu wa mkuu huyo wa wilaya kukutana mara kwa mara na makundi tofauti tofauti yaliyopo Wilayani humo ikiwemo Viongozi wa Dini na kueleza mambo yaliyofanywa na Serikali, ambapo wamesema jambo hilo linasaidia jamii kuwa na uelewa wa pamoja na kuweza kupuuzia upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu wachache ambao hawana mapenzi mema na Serikali.
0 Comments