Na Sabato Kasika
Ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, wasichana, na wanawake ni miongoni mwa matukio yanayoleta aibu kubwa katika familia na jamii kwa ujumla.
Watoto wanapata vipigo mara kwa mara, kukoseshwa mahitaji muhimu, na kuambiwa wasifichue uovu huo, huku wakiambiwa kuwa wataadhibiwa endapo watafunua siri.
Katika juhudi za kukabiliana na aina hiyo ya ukatili, wadau wa haki za wanawake na watoto wameunda kamati za uongozi zinazoshirikisha watoto.
Kamati hizi zinahusisha watoto katika juhudi za kupambana na ukatili wa kijinsia. Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni, Dar es Salaam, kinajihusisha na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kama vile ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni, pamoja na rushwa ya ngono. Kituo hiki kimeunda kamati za watoto mitaani ili watoto washiriki moja kwa moja katika vita dhidi ya ukatili huo.
Mwenyekiti wa kituo hicho, Twalib Fatma, amesema kuwa wameamua kuunda kamati za watoto baada ya kugundua kuwa ukatili mwingi hufanywa na ndugu wa karibu kama vile baba, mjomba, shangazi, na wengine ndani ya familia, lakini unafichwa.
"Tunaamini watoto hawa wataweza kushirikiana kusikiliza na kufuatilia matukio ya ukatili yanayowakabili, kutatua migogoro midogo midogo, na kuwasilisha masuala mazito kwa viongozi wakubwa," amesema Twalib.
Ameeleza kuwa, kama vile watu wazima wanavyokuwa na taratibu zao za kutatua migogoro, hata watoto wanahitaji kuwa na mfumo wa namna hiyo.
Kupitia uongozi wa watoto, anaamini kuwa itapanua wigo wa watoto hao kuripoti matukio ya ukatili ambayo yamekuwa yakifanyika ndani ya jamii.
"Tuliwakusanya watoto katika maeneo wanayocheza na kuwapa wazo hili, kisha tukawapa nafasi ya kuchagua viongozi wao. Sasa wana uongozi wao rasmi," amesema.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa mfumo huu utawasaidia watoto kuwa na njia ya kueleza matatizo yao kwa viongozi wa watoto wenzao, ambao watatoa taarifa zaidi kwa kituo hicho.
Watoto hao pia wamepewa mafunzo ya jinsi ya kushughulikia migogoro midogo midogo.
Fatma amesema kuwa kamati za watoto zitaanza kushughulikia kesi ndogo ndogo kama vile ugomvi wa kawaida kati ya watoto, ili kujenga uzoefu na umoja miongoni mwao.
0 Comments