NA WILLIUM PAUL, SAME.
WAKATI zoezi la uandikishaji Wananchi kwenye Daftari la Mkazi likiendelea, Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ameibukia kwenye Mnanda (ghulio) wa Kisiwani kuwahamasisha Wananchi kwenda kushiriki kujiandikisha ili waweze kupiga kura kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa kwenye Uchaguzi Novemba 27 mwaka huu.
Akizungumza na Wananchi hao, Kasilda amesisitiza kuwa baada ya kujiandikisha wahakikishe wanashiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi Novemba 27, kuchagua viongozi bora ambao watazibeba changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati.
“Kupiga kura ni haki yako mwananchi wa Kisiwani, lakini hakikisheni mnachagua watu ambao watawabeba na matatizo yenu kwa miaka mitano ijayo, maendeleo ya Kisiwani yataletwa na sisi wanakisiwani”. Alisema Kasilda.
Zoezi la uandikishaji Wananchi kwenye Daftari la Mkazi limeanza Oktoba 11 mwaka huu na linaendelea hadi kufikia Oktoba 20 ambapo wilaya ya Same kuna Vitongoji 503 ambapo kwa kila Kitongoji ni Kituo cha kuandikisha Wananchi kwenye Daftari la Mkazi.
0 Comments