Header Ads Widget

ACT WALIA RAFU UANDIKISHAJI DAFTARI LA MKAZI



Na Fadhili Abdallah,Kigoma       

 

CHAMA Cha ACT Wazalendo mkoa Kigoma kimetaka kusimamishwa kwa mchakato wa zoezi la uandikishaji wapiga kura katika daftari la mkazi wakilalamikia kuongezwa kinyemela kwa wapiga kura kwenye daftari hilo hali inayoeleza ili kuipa ushindi CCM kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27 mwaka huu.

 

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo jimbo la Kigoma Mjini, Halfan Bona akizungumza mbele ya waandishi wa Habari alisema kuwa wanao Ushahidi wa kufanyika kwa vitendo hivyo vibavyofanywa na waandikishaji wa vituo kwa maelekezo yanayotolewa na viongozi wa CCM.

 

Bona alisema kuwa ili kufanikisha hilo waandikishaji na wasimamizi wa vituo wamekuwa wakiwatoa nje mawakala wa vyama vya siasa na kuwazuia kuingia  kwenye vituo kwa madai mbalimbali ya uongo.

 


Akizungumza katika mkutano huo Mratibu wa uandikishaji jimbo la Kigoma Mjini wa Chama Cha ACT Wazalendo, Frank Luhasha alisema kuwa kutokana na ukiukwaji wa taratibu unaofanywa wameitaka serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI kusimamisha mchakato huo sambamba na kuwaondoa waandikishaji na watendaji wanaotuhumiwa.

 


Ruhasha alisema kuwa wanataka uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa uwe wa amani na huru lakini kwa hatua ambazo zimeanza kufanywa na wasimamizi wa zoezi hilo ni wazi inatia shaka uwepo wa uwazi na kufuatwa kwa taratibu kwenye uchaguzi huo.

 

Akijibu hoja hiyo Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Kigoma Mjini, Kisena Mabuba alisema kuwa hakuna uingizaji wa majina bandia unaofanywa katika zoezi hilo na kwamba kila chama kimetakiwa kuwa mawakala kwenye kila  kituo  ili kuhakiki zoezi zima.

 

Mabuba ambaye ni Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji alisema kuwa hata hivyo  vituo vingi havina mawakala wa vyama vya siasa  na hata waliopo hawakai vituo muda wote hivyo wanaporudi kwenye vituo na kukuta namba imeongeza wakati hawapo ndiyo wanaibua madai ya kuwepo kwa uingizwaji wa majina hewa.

 

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI