Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mbeya, kimewataka wananchi kutosusia suala la uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji kwa maelezo kuwa kura zao ndio zitakazoamua aina ya viongozi na hatma ya maisha yao ya miaka mitano (2024-2029).
Hayo ni kwa mujibu wa mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mbeya Masaga Pius Kaloli wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Chunya mjini mkoani Mbeya kwenye mwendelezo wa mikutano ya hadhara inayoendelea wilayani humo.
Masaga amesema wananchi wana hatma ya kuamua aina ya viongozi watakaowatumikia kwa kipindi cha miaka mingine mitano ijayo.
Amesema Serikali iliyoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeshindwa kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli kwani maendeleo yanayosemwa hayasadifu uongozi wenye dhamira ya kweli ndani ya miaka zaidi ya sitini tangu uhuru.
"Ndugu zangu watu wa Chunya na wa-Tanzania kwa ujumla, hatupaswi kususia uchaguzi huu (wa Serikali za mitaa) kwani Chama Cha Mapinduzi hatuwezi kukiondoa madarakani kwa bunduki kwasababu ni za kwao, hatuwezi kwa maneno wala nini isipokuwa tutakwenda kuwaondoa madarakani CCM kupitia sanduku la kura", amesema Masaga.
Kiongozi huyo wa CHADEMA mkoani Mbeya amesema Chunya inaendelea kukabiliwa na matatizo lukuki ndani ya miaka isiyopungua sitini ya uhuru hali anayosema imewachosha wananchi.
"Lakini pia Chunya chini ya CCM mpaka leo bado maji ni tatizo hadi mjini kwa wajanja hapa (Chunya mjini), huduma za afya ziko chini ya kiwango, agenda ya kuiondoa CCM madarakani sio lele mama maana CCM ndio imetuletea ugumu wa maisha", ameongeza mwenyekiti Masaga Kaloli.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Vwawa mkoani Songwe ambaye amehudhuria mkutano huo Mch. Amoni Tuloline Mwashitete, ametoa ole kwa wasimamizi wa uchaguzi watakaohujumu uchaguzi huo akisema hawatovumiliwa pamoja na mipango yoyote ya baadhi ya wagombea kupita bila kupingwa.
Katibu wa Chama hicho jimbo la Lupa wilayani Chunya Yohana Mpamba (Mcotton), amesema Chunya ni jimbo ambalo limedumaa kimaendeleo hivyo kuwataka wananchi kwenda kufanya mabadiliko chenye chaguzi zijazo kwa kuhakikisha wanapata viongozi bora watakaokuwa sauti yao.
Haya ni maandalizi kuelekea kufungwa kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura kwenye daftari la mkazi kwa ajili ya Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji na baadaye Novemba 27, 2024 ndipo uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji utafanyika kote nchini.
0 Comments