Waziri wa Maliasili na utalii Balozi Dkt Pindi Chama
NA MATUKIO DAIMA APP
WAZIRI wa Maliasili na utalii Dr Pindi Chana anatarajiwa Mgeni rasmi katika ufungaji wa Kilele Cha maadhimidho ya Miaka 60 ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha mkoani Iringa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Kuelekea maadhimidho hayo Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Godwel Ole Meing’ataki alisema maandalizi ya maadhimisho hayo yatatanguliwa na shughuli mbali mbali za kijamii pamoja na elimu juu ya umuhimu wa Hifadhi hiyo.
Alisema kuwa Hifadhi imejipanga kuimarisha uhusiano na jamii mbalimbali, ikiwemo watu wenye ulemavu, kwa lengo la kuwapatia fursa ya kutembelea hifadhi hiyo pamoja na kutoa msaada kwa familia zenye mazingira magumu
“Nitumie fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote, hususan wakazi wa Iringa, katika maadhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo yatafanyika kuanzia tarehe 1 hadi 7 Oktoba, 2024, huku kilele chake kikitarajiwa kuwa tarehe saba,” alisema Meing’ataki.
Alisema kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo Balozi Dkt. Chama ambaye atahitimisha shughuli hiyo kwa kuzindua rasmi utalii wa puto.
Kuwa huduma hii mpya ya utalii wa puto inalenga kuwavutia watalii zaidi katika hifadhi hiyo kwa kuwapa fursa ya kufurahia mandhari ya kuvutia ya Ruaha kutoka angani.
Alisema Katika maadhimisho hayo, Hifadhi ya Ruaha itashirikiana na wadau mbalimbali wa mkoa wa Iringa, wakiwemo viongozi wa kimila na kidini, kwa kufanya ziara maalumu za kutembelea hifadhi hiyo.
Meing’ataki alieleza kuwa ziara maalum kwa Chifu wa kabila la Wahehe na viongozi wake wa kimila, pamoja na viongozi wa dini, zimepangwa ili kuongeza uelewa na ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira.
Pia, alisema kutakuwa na kongamano maalum la miaka 60 ambalo litajikita katika kujadili historia ya hifadhi hiyo, mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizopo, sambamba na kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha uhifadhi.
Hifadhi hiyo pia imeandaa ziara kwa watu wenye ulemavu kutoka mkoa wa Iringa ili wapate fursa ya kutembelea na kujionea vivutio vilivyomo katika hifadhi ya Ruaha.
Aidha, wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hiyo, hasa wenye mazingira magumu, watapewa msaada na kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi maliasili na faida za kiuchumi zinazoweza kupatikana kutokana na utalii endelevu.
Katika hatua nyingine, Meing’ataki alibainisha kuwa kutakuwa na bonanza la michezo litakalofanyika katika eneo la Tungamalenga kwa lengo la kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi kupitia burudani.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana, Meing’ataki alisema Hifadhi ya Taifa ya Ruaha imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964.
Alisema awali, hifadhi hiyo ilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 9,500, lakini sasa imeongezeka na kufikia kilomita za mraba 19,822.
Hivyo Ongezeko hili limechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla hivyo Ruaha inajivunia kuwa na idadi kubwa ya wanyama wa aina mbalimbali.
Kwa sasa, hifadhi hiyo inakadiriwa kuwa na tembo wapatao 15,000, nyati 20,000, simba zaidi ya 8,000, pamoja na wanyama wengine na ndege wa aina mbalimbali. Hali hii imeifanya Ruaha kuwa moja ya vivutio muhimu kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
Meing’ataki aliongeza kuwa maboresho makubwa yamefanyika katika miundombinu ya hifadhi hiyo, ikiwemo maeneo ya mapokezi, malazi, na barabara, jambo ambalo limeongeza ufanisi katika kutoa huduma bora kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.
Mbali na kuwa kivutio kikubwa cha watalii, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pia ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.
Mto wa Ruaha, ambao unapita ndani ya hifadhi hiyo, ni chanzo muhimu cha maji kwa bwawa la Mtera, ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa umeme nchini.
Hivyo uhifadhi wa mto huo unasaidia kuhakikisha uzalishaji endelevu wa nishati ya umeme ambayo inategemewa na taifa.
Hifadhi ya Ruaha pia inachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya kigeni kupitia utalii.
Kuwa watalii wanaotembelea hifadhi hiyo hulipa ada mbalimbali za kuingia, malazi, na huduma nyinginezo, ambazo huingiza mapato makubwa kwa taifa.
Alisema katika kuelekea maadhimisho haya, Meing’ataki alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo kwa kutembelea hifadhi ya Ruaha.
Kuwa ni muhimu Watanzania, hususan watoto, wawe na utamaduni wa kupenda na kuthamini vivutio vya ndani ili kuunda kizazi chenye mwamko wa uhifadhi wa maliasili na urithi wa taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Iringa mjini Frank Nyalusi alisema maadhimisho hayo yatafungua fursa kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa Iringa hivyo hawana budi kuchangamkia fursa za kiutalii.
Alisema tayari ujenzi wa Barabara ya lami Kilomita 104 toka Iringa mjini Hadi Msembe katika lango la Hifadhi hiyo inajengwa pia Uwanja wa Ndege wa Iringa upo Mbioni kumalizika kuwa itachangia kukuwa kwa utalii.
Huku muongoza watalii Salafino Lanzi akieleza kuwa maadhimisho hayo ni fursa kwao kwani idadi ya watalii itaongezeka zaidi .
Maadhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yanaashiria hatua kubwa zilizopigwa katika sekta ya uhifadhi na utalii nchini hivyo no wakati muafaka kwa Watanzania wote kushiriki katika juhudi za kuendeleza na kulinda urithi wa asili wa nchi yetu kwa vizazi vijavyo.
0 Comments