Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
MWENYEKITI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) Mkoa wa Singida, Rajabu Mussa, amewataka wazazi,walezi na walimu kushirikiana katika kuimarisha malezi na maadili mema kwa watoto ili kujenga jamii nzuri ambayo itasaidia nchi katika kuleta maendeleo.
Akizungumza jana wakati wa mahafali katika Shule ya Msingi Nkwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida, alisema kama watoto hawatatengenezewa mazingira mazuri watoto wataingia mitaa na kujiingiza katika makundi mabaya ya wavuta bangi.
"Ndugu zangu wazazi leo hii tuna majanga makubwa sana wananchi wa Nkwae hivyo ni lazima tutambue kuwa watoto ni raslimali kubwa sana kwani ndio kizazi ambacho kinakuja kuishika jamii baada ya sisi kuondoka," alisema.
Mussa alisema maadili na tabia njema huchangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga na kuimarisha jamii yenye amani na umoja ambapo mtoto anapolelewa katika misingi ya maadili mema na tabia njema, inaimarisha uelewa na uwezo wake wa kupambanua matendo mema na mabaya.
Aliongeza kuwa wazazi pia wanajukumu la kuhakikisha watoto wao wanasoma kwani taifa ili liweze kuendelea ni lazima watu wasome ndipo maendeleo yatapatikana.
"Wapo watoto wanaona kutafuta pesa ni bora kuliko kusoma bila kujua kwamba taifa lolote ili liweze kupaata maendeleo kila kijiji na kila mtaa lazima watu wasome ndipo maendeleo yapatikane," alisema.
Mussa alisema kijiji kama hakitakuwa na wasomi au taifa lolote au kijiji ambalo halitakuwa na wasomi litakuwa limekufa kwani ni jambo la wazi kwamba maendeleo yanaletwa na wasomi.
Aidha, Mwenyekiti huyo alitahadharisha kipindi hiki wazazi kuwa makini na watoto wao kutoka na uwepo wa matukio ya ulawiti na ubakaji ambayo yameshika kasi kwa kuhakikisha wanachunguza watoto wao wanapokwenda na kurudi kutoka shule.
Kuhusu shule hiyo kukosa umeme, aliwahidi kuwa yeye kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji watawasiliana na Mkuu wa Wilaya kumjulisha changamoto hiyo ili umeme ufikishwe katika shule hiyo na hivyo kuwawezesha wanafunzi kusoma muda wote.
MWISHO
0 Comments