Header Ads Widget

RC DENDEGO ALIPONGEZA KANISA LA WAADVENTISTA WASABATO

 



Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 

MKUU wa Mkoa wa Singida,Mhe.Halima Dendego, amelipongeza Kanisa la Waadventista Wasabato kwa kujenga kituo ambacho kitakuwa kinasaidia kutoa mafunzo ya stadi za kazi waraibu wa dawa za kulevya,watoto wa mitaa na makahaba ili waweze kujikwamua kiuchumi.


Kituo hicho ambacho ujenzi wake bado unaendelea kinajengwa na kanisa hilo kuoitia dara ya wanawake kwa fedha zinazochangwa na wanawake kutoka nchi 11.

Mhe.Dendego ametoa pongezi hizo leo (Septemba 11, 2024) wakati akifungua mkutano wa kongamano la wanawake kanda ya Afrika Mashariki na Kati wa Kanisa la Waadventista Wasabato unaofanyika eneo la Ititi Manispaa ya Singida.


"Binafsi ninawapongeza sana kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa mwanamke katika jamii kwa kuwapa fursa ya kumtumikia Mungu na kuzisaidia jamii zetu,"amesema Mhe.Dendego.



Amesema ni ukweli mtu kuwa Mungu amewapa wanawake uwezo mkubwa na iwapo watatumia fursa kikamilifu familia,jamii,taifa na mataifa yatastawi kutokana na uwezo na vipawa vya kipekee ambavyo Mungu amewapa wanawake.


"Hapa kwetu Tanzania kuna usemi usemao Wanawake wakiwezeshwa wanaweza,ninataka wanawake wenzangu tutoke kwenye kifungo cha usemi huu hatuhitaji kuwezeshwa bali tunapaswa kujiamini kuzitambua fursa na kuweka jitihada zetu sisi wenyewe ili kuzitumia kwa manufaa yetu,jamii nanl taifa kwa ujumla," amesema Mhe.Dendego.


Ameongeza kuwa wanawake ndiyo chanzo cha jamii na walezi wa watoto na wanaume hivyo hakuna mafanikio katika jamii wala kwa mwanaume bila uwepo wa mwanamke imara nyuma yake.


Aidha, aliwakumbusha wanawake kutimiza kikamilifu jukumu la wazazi na walezi kwa kusimamia vyema maadili ya watoto wa kike na wa kiume.


"Sote tumekuwa mashuhuda wa athari zinazotokana na kumomonyoka kwa maadii kunakopelekea kuibuka kwa vitendo ambavyo ni kinyume cha mila,desturi na utamaduni wa kiafrika," amesema Mhe.Dendego.



Amesema kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anakemea na kupinga vitendo vya mahusiano ya jinsia moja kwani suala hili linaumiza jamii,linapoteza nguvu kazi ya taifa na ni haramu katika imani ya dini zote na dhambi kwa Mwenyezi Mungu.


Amesema hivi sasa limeibuka suala la usafirishaji haramu wa binadamu hususani walemavu ambao wanakwenda kutumika kama mitaji ya kuombea fedha .


"Niwaombe wanawake tusimame imara kulikemea hili kwani tukijisahau linaweza kushamiri na kujikuta katika jamii zetu tunasababishiana ulemavu wa makusudi," amesema Mhe.Dendego.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI