HUKU Chama Cha Demokrasia na maendeleo ( CHADEMA) ikidai kutekwa Mjumbe wa Sekretarieti ya chama hicho Taifa, Ally Mohamed Kibao akiwa kwenye usafiri wa umma, Jeshi la Polisi limesema limeanza uchunguzi kubaini kilichotokea, chanzo chake na watu waliohusika.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime leo Septemba 7, 2024 imesema jana Septemba 6, 2024 zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa jioni maeneo ya Tegeta jijini Dar es Salaam, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Ally Mohamed Kibao, akiwa safarini na basi la Tashrif alichukuliwa na kushushwa kutoka kwenye basi hilo na watu ambao hawakuweza kujulikana majina yao.
"Leo Septemba 7, 2024 tumesikia taarifa kuhusiana na tukio hilo kupitia vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, John Mnyika.
"Jeshi la Polisi, lingependa kutoa taarifa kuwa, lilipokea taarifa hiyo na kuanza uchunguzi wa kubaini kilichotokea, chanzo chake na watu waliohusika ni kina nani," imesema taarifa ya Polisi.
Aidha Katibu wa Chadema, John Mnyika akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 7, amesema taarifa za tukio hilo zilianza kusambaa Septemba 6 kupitia mitandao ya kijamii ikidaiwa saa 12.00 jioni Mohamed akiwa kwenye basi la abiria la Kampuni ya Tashrif akitoka Dar es Salaam kwenda Tanga eneo la Kibo Complex Tegeta basi lao lilizuiwa na magari mawili.
Katika magari hayo yaliyozuia basi hilo, inadaiwa watu wenye silaha walishuka na kupanda ndani ya basi hilo na kumkamata kisha kumfunga pingu.
0 Comments