NA WILLIUM PAUL, SAME.
MBUNGE wa Jimbo la Same mashariki wilaya Same mkoani Kilimanjaro, Anne Kilango Malecela amekuja na mkakati wa kufanya mikutano ya hadhara na wananchi wa Jimbo hilo mchana na usiku lengo likiwa ni kuzifikia kata 14 vijiji 49 na vitongoji 207 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Hii ni histori ya kipekee kwa viongozi wa kisiasa kufanya mikutano ya hadhara nyakati za usiku ambayo amekuja nayo Mbunge huyo.
Zoezi hilo lilianza jana ambapo majira ya saa mbili usiku alifanya mkutano wa hadhara kwa wananchi wa kijiji cha Mweteni kata ya Bwambo ambapo mamia ya wananchi walijitokeza katika mkutano huo.
Mbunge Anne alisema kuwa, lengo la kufanya mikutano usiku na mchana ni kuhakikisha anawafikia wananchi wote wa Jimbo la Same mashariki na kueleza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mkutano huo ulifungwa majira ya saa nne za usiku ambapo Mbunge huyo pamoja na jopo aliloongozana nalo waliamua kulala nyumbani kwa Katibu wa Tawi la Ndambwe kijiji cha Mweteni, Stanley Tumaini.
Jambo hili limepokelewa kwa hisia kubwa kwa wananchi ambapo wamefurahishwa kuona Mbunge huyo ameshuka na kuishi maisha yao wanayoyaishi kila siku.
Mwisho.
0 Comments