Na MWANDISHI WETU
Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Othman Masoud Othman amesema Mapinduzi ya Mwaka 1964 hayakufuta Mamlaka kamili ya Zanzibar ya kuwa na kiti cha dola Umoja wa Mataifa na badala yake yaliweka utaratibu wa uwendeshaji wa Serikali.
Othman Masoud ameyasema hayo wakati akihutubia Wananchama wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja Jongomeo Chambani,Wilaya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.
“Mapinduzi yalipokuja hayakuja kupindua dola ya Zanzibar yalikuwa yalikuja kubadilisha mfumo wa kuendesha dola ya Zanzibar na ndio maaana kiti chake umoja wa mataifa kilibaki kilekile Umoja wa Mataifa,”.
Alisema ndio maana Rais wa Kwanza wa Zanzibar baada ya mapinduzi aliteuwa baraza la mawaziri kama kawaida na balozi wa kuiwakilisha Zanzibar katika baraza la Umoja wa Mataifa katika kulinda Mamlaka ya dola ya Zanzibar.
Alisema mbali uwakilishi Umoja wa mataifa Zanzibar iliendelea kuteuwa mabalozi wa kuiwakilisha nchi mbalimbali kwa sababu ilikuwa na mamlaka kamili kama nchi kabla ya kuzaliwa kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar 1964.
Aidha alisema kwa Wananchi wa Chambani ni alama kubwa inayohitaji kuenziwa kwa sababu Mzanzibar wa kwanza alie ratibu na kusimamia suala la Zanzibar kuwa Mwanachama wa umoja wa mataifa ni Waziri Mkuu wa kwanza baada ya mapinduzi Mohammed Shamte ambae alikuwa mzaliwa wa chamabani Mkoa wa Kusini Pemba.
“Kama kungekuwa tupo katika nchi ambayo inahifadhi historia yake na kuthamini chambani tungejenga mnara wa kumbukumbu wa kuenzi wana chambani, alichokifanya ni alama kubwa ya kwenda kusimamisha Zanzibar kama dola katika Mamlaka ya kimataifa,”
Akizungumzia tatizo la ajira alisema Serikali imepoteza uwezo wa kuajiri vijana kwa sababu hakuna uwiano kati ya mapato yanayokusanywa na Serikali kwa mwaka na ukubwa wa tatizo la ajira kwa vijana Zanzibar.
“Serikali hii inakwenda kukusanya Trilioni 1.5 na bilioni 900 zinakwenda kulipa mishahara na Bilioni 300 zinakwenda kulipa madeni mbali na gharama za uendeshaji,”
Othman ambae ni makamu wa kwanza wa Rais alisema takwimu zinaonesha kila Mazanzibar kwa mwezi anachangia mshahara wa watumishi wa umma shilingi 41,000 wakiwemo Watoto wakati Tanzania bara kila mwananchi akichangia Shilingi 15,000.
Alisema hakuna nchi yoyoyte duniani inayotumia mapato yake asilimia 65 kulipa mishahara na iweze kutoa ajira kwa wananchi wake mbali na fedha za kulipa madeni.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Act Wazalandio Taifa Omar Ali Shehe ametangaza rasmi haki za msingi wanazozipigania chama hicho ikiwemo Wananchi kupata huduma bora na kila mwananchi kupata haki ya kikatiba ya kuishi pamoja na Zanzibar kuwa mwanachama umoja wa mataifa.
“Tunapigania haki ya kuchagua viongozi wanaotuongoza wakiwemo madiwani,wawakilishi, wabunge na Rais,tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi wazanzibar tunateseka na kuongozwa na watu tuisowataka kuanzia majimbo hadi serikali,”
Chama cha Act Wazalendo kinaendelea na mikutano yake ya hadhara huku wakitumia muda mwingi kukosoa misingi ya Demokrasia na uwatala bora licha ya kuwemo katika Serikali ya umoja wa kitaifa huku wakilalamika kuongezeka kwa ukali wa Maisha na kuwapa ugumu wananchi wenye kipato cha chini.
0 Comments