Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Halmashauri ya mji wa Njombe imeweka wazi mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa kuwa Novemba mosi hadi 7 Mwaka huu zitatolewa fomu za uchaguzi kwa wagombea na Kuzirejesha kisha utafuatia mchakato wa uteuzi.
Akitoa maelekezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa mbele ya wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa, wananchi na kundi la maofisa usafirishaji Bodaboda na Bajaji mjini Njombe Msimamizi mkuu wa uchaguzi Kuruthum Sadick ambaye ni mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Njombe amesema Kampeni za uchaguzi huo zitaanza Novemba 20 hadi 26 kuanzia majira ya saa mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni na hii ni kwa mujibu wa kanuni Ya 27 GN 573 na 574.
Aidha Kuruthum amesema pia mapingamizi yoyote yatakayowekwa yatasikilizwa katika kipindi cha siku sita.
Baada ya maelekezo hayo kituo hiki kimezungumza na makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa huku Ally Mhagama katibu mwenezi wa ACT Wazalendo mkoa wa Njombe na Lukule Mponji mwenyekiti wa TLP Wakiwa na hofu ya uchaguzi huo kwa kuwa wasimamizi sio Tume huru ya uchaguzi.
Singo Ndoela ni kaimu katibu wa CCM Wilaya ya Njombe ambaye amewataka viongozi wa vyama vya upinzani kuondoa mashaka juu ya uchaguzi huo kwani Rais aliahidi kuendesha uchaguzi wa huru na haki.
Kwa upande wao baadhi ya Viongozi wa dini wamesema hatua ya serikali kuwashirikisha katika mchakato huo itasaidia kuwapa taarifa sahihi waamini wao huku wakishauri vyama vya upinzani kufuata sheria katika malalamiko yao.
Waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa Alitangaza Novemba 27 mwaka huu kuwa ni tarehe ya Uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo makundi yote yenye sifa ya kuchagua na kuchaguliwa yanayo nafasi ya kushiriki katika zoezi hilo.
0 Comments