Header Ads Widget

DC MACHALI - VIONGOZI WA DINI MSAIDIE KUELIMISHA WANANCHI KUSHIRIKI UCHAGUZI

 

Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 

MKUU wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali, amewataka viongozi wa dini wilayani hapa kutumia vyema nafasi zao kuelimisha wananchi kuhusu kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kuhubiri maadili mema nchini.

Alisema hayo jana wakati wa kikao na viongozi wa dini ambacho kilikuwa na lengo la kujadili masuala yanayohusu mmomonyoko wa maadili,  uzalendo, amani pamoja na ushiriki wa viongozi hao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

“Ningependa kutumia nafasi hii kuwataka mkawaeleze waumini kuhusu kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakofanyika Novemba 27, 2024 kwa amani na upendo. Tujitokeze kwa wingi katika kampeni, tujiandikishe kwenye daftari la orodha ya wapiga Kura na siku ya uchaguzi tuchague viongozi wetu kwa amani," alisema.

Aidha, Machali aliwakumbusha viongozi hao wa dini kuhusu zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutumia nafasi zao kuwaeleza wananchi ifikapo Septemba 25,2024 wajitokeze kuboresha taarifa zao kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa  2025.

Akizungumzia kuhusu suala la maadili  alisema viongozi wa dini wanajukumu kubwa katika kuhubiri amani pamoja na kulinda maadili ya jamii za kitanzania.

"Twendeni tukahubiri amani na upendo kwa waumini wetu, nitashangaa siku nikisikia watu wa Mkalama wanagombana kwasababu ya dini, kila mmoja aheshimu imani ya mwenzake," alisema.

Naye Mchungaji Manase Msengi, kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Ushirika wa Nduguti, akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake alimshukru  na kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama kwa kukutana na viongozi wa dini kwa ajili ya kujadili masuala ya maadili, uzalendo na amani hasa katika kipindi hiki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwataka wananchi wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI