Polisi imesema imebaini kuwepo kwa mipango haramu ya viongozi wa chama cha siasa nchini ambacho ni CHADEMA kuhamasisha vijana kote nchini kukusanyika katika mkoa wa Mbeya Agosti 12, 2024 kwa lengo la kufanya maandamano na mikusanyiko kwa mwamvuli wa maadhimisho ya siku ya vijana duniani.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo ya Polisi makao makuu ya Polisi Dodoma CP Awadh Haji, hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii wameonekana na kusikika baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakihamasisha vijana kote nchini, viongozi wa kitaifa wa chama, kamati kuu ya chama hicho na kualika baadhi ya watu kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kuadhimisha siku ya vijana Mkoani Mbeya.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya polisi kwa umma kupitia vyombo vya habari, pamoja na mwaliko wanaotoa, viongozi hao wameendelea kutoa kauli ambazo zinadaiwa kuwa hazionyeshi kuwa na lengo la kwenda kuadhimisha siku ya vijana duniani bali ni kwenda kuhamasisha kufanya vitendo vinavyolenga uvunjifu wa amani kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya.
Cp Awadh, amesema miongoni mwa kauli hizo ambazo zinaashiria kuwa na lengo la kuvuruga amani ni za Katibu Mwenezi BAVICHA Taifa Twaha Mwaipaya aliyenukuliwa akisema “Kama kijana yeyote unaipenda nchi yako ya Tanzania, umeshalia miaka yako yote, siku hiyo ya tarehe 12/08/2024 tunakwenda kuweka hatma ya Taifa letu la Tanzania mkoani Mbeya, kwa hiyo kijana yeyote uliyepo popote Tanzania njoo uwanja wa Ruanda Nzovwe Mbeya”, amesema kamishna huyo wa Polisi na kuongeza kuwa kauli nyingine ni kuwa “Tupo serious sana na jambo hili, kwa hiyo vijana wote wa CHADEMA kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua, siku ya tarehe 12/08/2024 tunakwenda kuacha uteja kwa Serikali, vijana wa kitanzania na kuweka maazimio makubwa ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025”, amesema kamishna Awadh akinukuu baadhi ya kauli zinazodaiwa kutolewa na katibu mwenezi wa BAVICHA Taifa Twaha Mwaipaya.
Ameeleza kuwa kauli hizo ni viashiria tosha kuwa malengo yao sio kwenda kuadhimisha siku ya vijana duniani bali ni kuanzisha na kufanya vurugu ili kusababisha uvunjifu wa amani nchini vitendo ambavyo haviwezi kuvumiliwa na Polisi wenye jukumu la kuhakikisha ulinzi na usalama wa jamii.
Kufuatia kauli na matamko mbalimbali yanayotolewa na viongozi hao, Jeshi la Polisi nchini Tanzania limeamua kupiga marufuku maandamano na mikusanyiko ya aina yoyote ile ya ndani au nje inayotaka kufanyika kwa mwamvuli wa kuadhimisha siku ya vijana duniani ikilenga kuleta uvunjifu wa amani mkoani Mbeya na nchini kwa ujumla hivyo Polisi imetoa onyo na katazo kwa mtu au kikundi cha watu kinachojipanga kufanya maandamano na mikusanyiko kuacha mara moja kwani Jeshi la Polisi lipo imara na limejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi, usalama, amani na utulivu vinatawala nchini na lipo tayari kuzuia na kupambana na viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani lasivyo hatua zitachukuliwa kwa watakaokiuka maelekezo hayo.
0 Comments