Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Zanzibar imekwama kiuchumi na wananchi wake kuendelea kuishi kwenye umasikini wa kutupwa kutokana watawala wa Chama Cha Mapinduzi kukosa dira na maono ya namna bora ya kuendesha nchi na badala yake kujikita kwenye kutumia madaraka yao kujinufaisha binafsi.
Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo jana Jumamosi, Agosti 10, 2024 wakati alipokuwa akiwahutubia viongozi, wanachama, wapenzi na wafuasi wa Chama chake, akiwa Mgeni Rasmi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Uwanja wa Mwambao, Kwa Ayuba, Jimbo la Magomeni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
"Hawa wameshajibainisha kwamba hawawezi kuongoza nchi hii badala yake ni kujinufaisha wao binafsi", amesisitiza Mheshimiwa Othman.
Akipigilia msumari hoja yake, Mheshimiwa Othman alisema ni aibu na fedheha kubwa kwa Zanzibar ambayo ni nchi yenye historia kubwa ya uchumi imara, biashara huru na mahusiano ya kimataifa na madola makubwa ulimwenguni kwamba leo ipitwe kwenye maendeleo na maisha mazuri ya watu na nchi nyingine za visiwa kama Seychelles, Mauritius na Maldives.
Akitoa mfano amesema ni aibu na fedheha kuona baada ya miaka 60 tangu Zanzibar iwe huru bado wananchi wanakosa maji safi na salama kwa wakati.
Akikazia hoja zake, Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo alisema mbali na kukosa uongozi wenye dira na maono, sababu nyingine kubwa inayoikwamisha Zanzibar kupiga hatua kubwa za maendeleo ni kutokana na kukosa mamlaka kamili kwa nchi huku ikiwa haina uwezo wa kusimamia wala kufanya maamuzi kwa mambo zaidi ya 41 ambayo yamedhibitiwa na Muungano usio wa haki.
Mheshimiwa Othman amewataka viongozi waliopo madarakani wajibu hoja zao inavyotakiwa na siyo maneno ya kipuuzi. "Tunatakiwa tuishi kwa hoja sio kutoa maneno yasiyofaa, na kama ni kweli muna dhamira ya kweli, jibuni hoja zetu", alisema.
Akihutubia hadhara hiyo Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Zanzibar), Ndugu Ismail Jussa, amesema ikiwa watawala wa CCM waliopo wanadai ufisadi unaoibuliwa na ACT Wazalendo ni uzushi na uongo basi anawataka wakubali waletwe wakaguzi huru wa kimataifa ili wachunguze miradi inayoitwa ya maendeleo iliyopo na kubainisha nani anasema kweli.
Huku akiorodhesha miradi 28 chini ya Serikali ya Awamu ya Nane aliyoisema kuwa imejaa ufisadi, alisema "kama kweli mnajiamini kubalini waje wakaguzi huru wa kimataifa wakague miradi hii, na kama hilo hamliwezi basi kaeni kimya".
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo, Mansoor Yussuf Himid, amesema Vijana wa Zanzibar wanatakiwa kurithishwa taifa hili likiwa na mapenzi, umoja, mshikamano na maridhiano ya dhati na sio chuki.
Akifafanua kauli hio, Mansoor amesema "wazazi wetu walioasisi nchi hii waliiendesha katika misingi ya umoja, mshikamano, mapenzi na silka njema lakini sasa tumefikishwa katika hatua ambayo ndugu zetu wa vikosi vya ulinzi vya Zanzibar wanatumika kuhujumu ndugu zao ili tu kuwaweka watawala madarakani hata kwa njia za dhulma, jambo ambalo ni hatari kubwa sana".
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo na Waziri wa Biashana na Maendeleo ya Viwanda, Mhe. Omar Said Shaaban, amesema hakuna mwenye mamlaka ya kuwazuia viongozi wa chama hicho kuhoji mapato na matumizi ya fedha za umma kwani ni haki yao na bado wataendelea kuhoji na kutaka majibu sahihi.
Akitoa salamu za wananchi wa Kusini Unguja Bi. Ziada Mwadini Mussa, amesema kinachotakiwa ni CCM kutambua kwamba umma umewakataa kwa sababu baada ya muda wote waliokaa madarakani, njama zao ovu, hila na ghilba zao tayari zimeshajulikana hata kwa wale waliokuwa wakiwaamini.
Viongozi wa ngazi mbali mbali wa Chama hicho wakiwemo Wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu, wamehudhuria mkutano huo wakiongozwa na Katibu wa Habari na Uenezi wa Chama hicho Taifa, Ndugu Salim Bimani.
0 Comments