Header Ads Widget

DKT. TULIA AFUNGUKA MAKUBWA YALIYOFANYIKA MBEYA MJINI, 'TUNAWANYOOSHA'.

 


NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Mbunge wa jimbo la Mbeya mjini Dkt. Tulia Ackson, amesema kazi yake ni kuendelea kufanya kazi ya kuwawakilisha wananchi na kupigania maendeleo yao na sio kupiga kelele kama wanavyofanya baadhi ya wanasiasa.


Dkt. Tulia ambaye pia ni spika wa bunge la Tanzania, amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa mtaa wa Shewa kata ya Mwakibete jijini Mbeya kwenye mkutano wake wa hadhara na wananchi wa kata hiyo.


Amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo jijini Mbeya ikiwemo kwenye kata ya Mwakibete.


Amesema wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa na kauli kwamba miradi kadhaa waliianzisha wao ikiwemo mradi wa maji kutoka chanzo cha mto Kiwira na barabara ya njia nne jijini humo kitendo anachosema kama mtu aliahidi na hakikutekelezeka ni upigaji kelele.


"Ndugu zangu wana Mwakibete niwaambie wako watu watakuja hapa oooh mradi huu wa Kiwira mimi ndiye nilianzisha sasa kwanini haukukamilika ujue ni kelele tu debe tupu! Atasema oooh mradi wa njia nne hapa mjini (Mbeya) ni mimi nilianza sasa kwanini hukuanza ujenzi mpaka Tulia ameingia ujue ni wapiga kelele debe tupu na niwaambie tunawanyoosha kweli kweli, hapa nimesema tu kwenye afya na elimu mambo yaliyofanyika", ameeleza Dkt. Tulia Ackson, Mbunge wa Mbeya mjini.



Pia ameeleza miongoni mwa miradi iliyotekelezwa ni kwenye sekta ya afya ambayo kata hiyo haikuwa na kituo cha afya, kuboreshwa kwa sekta ya elimu, maji na miundombinu ya barabara ambayo pamoja na lami kadhaa kujengwa ameahidi kuendelea kuboresha miundombinu hiyo.


Amewatoa hofu wananchi wake hao juu ya kero ambazo bado zinazowakabili kwa maelezo kuwa kama miradi mbalimbali ilivyotekelezwa ataendelea kuwapambania hivyo wasikubali kudanganywa na baadhi ya wanasiasa ambao ni wapiga kelele na sio watekelezaji wa mambo.



Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbeya mjini Afrey Nsomba, amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kumuunga mkono Mbunge wa Mbeya mjini Dkt. Tulia Ackson ili kutekeleza wajibu wake ipasavyo katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli kama ambavyo CCM iliahidi kwenye ilani yake ya uchaguzi.


Nsomba amewataka wananchi kuendelea kuiamini Serikali kwakuwa inashughulikia matatizo yanayowasibu ili kuleta ustawi wao na Taifa kwa ujumla.



Naye Diwani wa kata ya Mwakibete Lukas Mwampiki, amesikika akisema chama chake cha zamani (CHADEMA) ni wahuni ndio maana walishindwa kuleta maendeleo licha ya kuongoza Halmashauri ya jiji la Mbeya kwa miaka kumi tofauti na maendeleo yaliyoonekana ndani ya miaka minne ya CCM Mbeya mjini na katani kwake.


Ametumia hadhara hiyo kuwaomba wana CCM na wananchi kwa ujumla kujiandaa vizuri kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa kuhakikisha wanaichagua wagombea kupitia CCM ili kutochanganya betri na magunzi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI