Header Ads Widget

KAMATI YA BUNGE YA BAJETI KUUPA MSUKUMO MRADI WA MAFUTA GHAFI

 


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti leo wamekagua utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika kituo kitakachotumika kupokea, kuhifadhi na kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda ambapo wameahidi kuzidi kuupa msukumo mradi huo wa kimkakati katika mageuzi ya kiuchumi.


Baada ya kukagua kituo hicho kilichopo Kata ya Chongoleani wilayani Tanga, Mkoa wa Tanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Oran Njeza, amesema kamati hiyo ambayo inasimamia mipango na uchumi wa nchi imeona mradi wa EACOP una umuhimu kiuchumi hivyo wataendelea kuupa msukumo mkubwa ili ukamilike kwa wakati.


Kamati hiyo imempongeza, Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mabadiliko ya kiuchumi anayoyafanya kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama wa EACOP ambayo inaendana na jinsi dunia inavyokwenda kwa sasa.


"Mradi mkubwa kama wa EACOP haukutegemewa kufanyika kwenye nchi za kiafrika lakini maono ya Viongozi Wakuu wa nchi Uganda na Tanzania yamepelekea mradi huu kufanyika ili kuwezesha mafuta sasa kusafirishwa kwa njia ya mabomba ambayo pia yanasaidia katika ulinzi wa mazingira", amesema Mhe. Njeza.


Aidha, Kamati ya Bajeti imeitaka Wizara ya Nishati kuweka kipaumbele katika ujenzi wa mabomba  yatakayosafirisha nishati ya aina mbalimbali ikiwemo Gesi na Mafuta na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kituo cha usafirishaji wa nishati hizo barani Afrika.


Vilevile, kamati hiyo imeliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza nguvu ya kuutangaza mradi huo ili wananchi wafahamu jinsi Serikali inavyoendelea kutekeleza miradi yake. 


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema kuwa mradi wa EACOP unafaida mbalimbali katika mkoa huo ikiwemo kutoa ajira takriban 900, kuongeza mzunguko wa fedha, kuongeza fursa za biashara ikiwemo katika kituo cha kupokelea, kuhifadhi na kusafirikisha mafuta kilichopo Chongoleani Tanga, kuuza raslimali kama vile saruji na  kupata mapato mbalimbali kupitia ushuru.


Pia kiongozi huyo ametilia mkazo masuala ya afya na usalama pahala pa kazi katika miradi mbalimbali nchini ambapo ameipongeza EACOP kwa kutekeleza suala hilo kwa ufanisi ambapo katika masaa zaidi ya milioni mbili waliyofanya kazi hakuna ajali iliyotokea kwenye maeneo yao ya kazi.


Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio alisema mradi wa EACOP ni wa kielelezo na kimkakati kutokana na faida zake mbalimbali ikiwemo kuongeza mapato ya nchi katika kipindi cha ujenzi na uendeshaji kwa kiasi cha shilingi trilioni 2.3, kutoa ajira kwa watanzania ambapo mpaka leo umeajiri  takriban wananchi 7,584 huku ajira hizo zikitarajiwa kuongezeka.


Aliongeza kuwa kampuni 146 za kitanzania zimehusika kutoa huduma mbalimbali kwenye mradi na kunufaika kwa takriban Dola za Kimarekani milioni 246 na pia mradi umepelekea kufanyika kwa manunuzi ya Dola za Marekani milioni 462  pamoja na vijana wa kitanzania kupata mafunzo ya teknolojia mbalimbali ambapo ujuzi huo watautumia kwenye miradi mingine ya ujenzi wa mabomba kuelekea mbalimbali kama Kenya na Zambia.


Ametaja wanahisa wa mradi huo kuwa ni Kampuni ya Total Energies ya Ufaransa (62%), CNOOC ya China (8%), Kampuni ya Mafuta ya Uganda (15%) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (15%).


Amesema kwa ujumla mradi unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia 39.2 huku baadhi ya kazi zikikamilika kwa asilimia 100 ambapo ujenzi wa kiwanda cha kuwekea mabomba mfumo wa kuhifadhi joto cha Sojo ukifikia asilimia 90 na katika eneo la Chongoleani mradi umefikia asilimia takriban 40 na kueleza kuwa mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2026.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI