NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Kanda ya Nyasa kimewataka wananchi kwenda kuchagua viongozi bora kupitia Chama hicho kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa madai kuwa kwa sasa viongozi wa mitaa na vijiji wameshindwa kufanya kazi ikiwemo kusoma mapato na matumizi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa CHADEMA kanda ya Nyasa Gwamaka Mbughi wakati akihutubia wananchi wa kijiji cha Izumbwe kata ya Igale wilayani Mbeya kwenye mkutano uliofanyika Izumbwe mnadani.
Gwamaka amewaomba wananchi kuhakikisha wanajiandikisha kwenye daftari la mkazi na daftari la mpiga kura wakati utakapowadia ili kupata fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa maendeleo yao akiwasihi kuachana na Chama Cha Mapinduzi CCM akidai kimeshindwa kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli zaidi ya kuwadumaza na kufanya maisha yao kuendelea kuwa magumu.
Pia amesema Serikali iliyopo madarakani inaendelea kuwarundikia michango mbalimbali wananchi ikiwemo kodi, tozo na ushuru kwenye maeneo mbalimbali bila kuwa na uwezeshaji mazingira ya kufanyia shughuli za wananchi.
Kiongozi huyo mtendaji wa CHADEMA kanda ya Nyasa amesema Tanzania ina raslimali lukuki ambazo ni za kipekee lakini kutokana na uongozi mbovu raslimali hizo hazina tija yoyote ya kubadilisha maisha ya wananchi badala yake wanaendelea kuteseka na kuwa na hali ngumu hasa kiuchumi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Mbeya vijijini Getruda Japhet Lengesela, amewaomba wananchi wa kata ya Igale na Mbeya vijijini kwa ujumla kuhakikisha wanaichagua CHADEMA kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ili kupigania maslahi yao akidai viongozi waliopo sasa ni chanzo cha wao (wananchi) kuwa na maisha magumu.
Getruda anasema maisha yamekuwa magumu, huduma mbovu zinazotolewa kwa jamii, ushuru usio na utaratibu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye usafirishaji wa mazao na kwenye biashara ndogondogo na matatizo mengineyo kadhaa.
Mwenyekiti wa Baraza la wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) kanda ya Nyasa Tabia Kilasi Mwakikuti, amesema Chama Cha Mapinduzi kimechoka kwani kimeongoza zaidi ya miaka sitini hivyo wa-Tanzania lazima wafanye mabadiliko kwenye chaguzi zijazo lasivyo wataendelea kuteseka katika nyanja mbalimbali.
0 Comments