NA HAMIDA RAMADHAN MATUKIO DAIMA APP DODOMA
KWA mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 100 kama mtaji wa kuwezesha MSD kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na kukabiliana na changamoto za mnyororo wa ugavi.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai amezungumza hayo leo jijini Dodoma na Wahariri wa vyombo vya habari wakati akielezea mafanikio ya Bohari ya Dawa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 (Picha na Manase Madelemu)
Amesema Fedha hizo zimesaidia MSD kuwa na uwezo wa kuhudumia mahitaji ya vituo kwa wakati na kuweza kutengeneza mikakati ikayofanya taasisi iweze kununua kwa tija na kuimarisha Mahusiano na wazabuni mbalimbali.
Aidha ameeleza kuwa hadi kufikia Juni 2024 Bohari ya Dawa imepata mafanikio mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake.
"Mafanikio hayo yamepatikana katika maeneo kama yafuatayo kuongezeka kwa utimizaji wa mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya,Kuongezeka mizunguko ya usambazaji wa bidhaa za afya,kuimarika kwa makusanyo ya fedha kutoka vituo vya kutolea huduma za afya,kuongezaka kwa mapato ya MSD"ameeleza.
Aidha Mavere ameelezea mikakati kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kuwa ni pamoja na kuongeza ufanisi,kuimarisha mifumo ya kiutawala na kuongeza uwezo wa kifedha
Katika hatua nyingine ameeleza Ujenzi wa Maghala ya Kuhifadhi Bidhaa za Afya ambapo amesema kutokana na uwekezaji mkubwa wa serikali kwenye ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya, ongezeko la fedha za ununuzi wa bidhaa za afya na uwekezaji kwenye vifaa tiba, mahitaji ya miundombinu ya kuhifadhia bidhaa za afya yameongezeka.
"Kwa kutambua ongezeko hilo, serikali kupitia Bohari ya Dawa imeanza ujenzi wa maghala ya kisasa katika Kanda ya Mtwara na Dodoma ili kukidhi upungufu uliojitokeza na Ujenzi huu ukikamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 40,"
Na kuongeza "Kwa sasa mradi umefikia asilimia 55 kwa ghala la Mtwara na asilimia 58 kwa ghala la Dodoma ambapo Kukamilika kwa ujenzi wa maghala kutasaidia kuimarisha uhifadhi wa bidhaa za afya kwenye viwango stahiki, kusogeza huduma karibu na vituo vya kutolea huduma za afya, kupunguza gharama za uhifadhi na kuimarisha utunzaji wa bidhaa za afya, " Ameeleza Mkurungenzi huyo
Amesema Ujenzi huo wa maghala unatarajia kuongeza nafasi ya uhifadhi wa bidhaa za afya kwa mita za mraba 12,000 ambapo kwa ghala lililopo Dodoma mita za mraba 7,200 zitaongezeka na ghala la Mtwara kiasi cha mita za mraba 4,800 zitaongezeka hivyo kufanya ongezeko la uhifadhi kutoka mita za mraba 56,858.57 na kufikia mita za mraba 68,858.57.
0 Comments