*DODOMA*
Mtaalamu wa masuala ya uchimbaji, utafiti na uthaminishaji wa madini kimataifa pamoja na mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ya Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano Tanzania Mheshimiwa Neto Paul Kapalata, amelitaka Shirika la Uchimbaji Madini la Taifa (STAMICO) kuweka mkakati wa kimataifa utakaoliwezesha kushiriki katika mnyororo wa thamani wa uchumi mkubwa wa madini na kushindana na makampuni makubwa ya madini kimataifa, ikiwemo Barrick Gold Corporation, AngloGold Ashanti na kadha wa kadha kwa kuzingatia azma ya maono ya kufikia ubora wa Wizara ya Madini ifikapo 2030.
Akizungumza katika kikao cha pili cha kamati hiyo ya kudumu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Pius Msekwa, Bungeni, jijini Dodoma leo Januari16, 2026, Mheshimiwa Kapalata amesema STAMICO ina kila sababu ya kujipanga kitaasisi, kiteknolojia na kimtaji ili kuwa mdau mkubwa katika uchimbaji wa madini kwa viwango vya kimataifa, hatua itakayoongeza mchango wake kwa serikali na jamii kwa ujumla na kutojikita katika kuwekeza zaidi katika utoaji wa huduma za kitaalamu au vinginevyo za madini kwa angalizo kuwa itakuwa inashindana na wananchi wanaotoa huduma hizo hizo ambazo nyingi zimetengwa kwa ajili ya kundi linaloshirki katika sekta hii la ujumuishi wa *local content*.
Amesisitiza kuwa uzoefu wake wa ndani na nje ya nchi katika sekta ya madini utatumika kinagaubaga kama mjumbe wa kamati hiyo ili kujenga STAMICO mahiri yenye ushindani, ufanisi na uwezo wa kushiriki moja kwa moja kwenye miradi mikubwa ya uchimbaji wa madini, badala ya kubaki kwenye miradi midogo pekee.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Kapalata ameipongeza Wizara ya Madini kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika katika kuimarisha sekta hiyo nchini, akibainisha kuwa maboresho ya Sera, Sheria na usimamizi yamezaa matunda mengi ukilinganisha na nchi zingine barani Afrika.
Pia, ameahidi kuendelea kutoa ushauri na mchango wake kupitia kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua na kuchangia ipasavyo katika Pato la Taifa na maendeleo ya endelevu ya sekta.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Subira Mgalu, amempongeza Mheshimiwa Kapalata kwa mchango wake wa kitaalamu na ushauri wenye tija, akisema kuwa mawazo hayo ni muhimu katika mchakato wa kuijenga STAMICO imara, yenye manufaa mapana kwa Serikali, jamii na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Naye, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amempongeza Mhe. Kapalata kwa kushirikisha uzoefu wake mpana wa ndani na nje ya nchi katika sekta ya madini na kuahidi kuwa Wizara ya Madini itaufanyia kazi ushauri huo kwa lengo la kuimarisha STAMICO na kuiwezesha kushiriki kikamilifu katika uchimbaji mkubwa wa madini nchini na kimataifa.










0 Comments