Header Ads Widget

WANANCHI MAMBA KUSINI WAFURAHIA UPATIKANAJI WA FEDHA ZA UJENZI NA UKAMILISHAJI WA ZAHANATI ZA KIMANGARA NA LEKURA

 


Na WILLIUM PAUL, MOSHI. 


WANANCHI wa Kata ya Mamba Kusini iliyopo Jimbo la Vunjo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi  mkoani Kilimanjaro wamefurahia kupata fedha za ujenzi na ukamilishaji wa zahanati mbili za Kimangara na Lekura zilizoanza ujenzi kwa nguvu za wananchi tangu mwaka 2001. 


Wananchi hao wameonyesha furaha yao katika mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Dkt.Charles Kimei katika ofisi ya kijiji cha Lekura ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake kata kwa kata kusikiliza kero za wananchi pamoja na kueleza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi.



Zahanati ya Kimangara imetengewa shilingi milioni 90 na Lekura shilingi milioni 75 ambapo mpaka sasa wameshapokea shilingi milioni 25 kwa Kimangara na shilingi milioni 50 kwa Lekura. 


Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Kata wa kata hiyo mara baada ya kupokea fedha hizo walishaanza uundaji wa kamati za ujenzi, manunuzi na mapokezi ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuanza ujenzi katika zahanati hizo. 



Kupatikana kwa fedha hizo kumetokana na jitihada za Diwani wa kata hiyo Elirehema Tesha na Mbunge wa Jimbo la Vunjo Dkt Charles Stephen Kimei za kuwaletea maendeleo katika kata hiyo kwa kushirikiana na Serikali ikiwa ni utekelezaji wa vitendo wa ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 - 2025.


Akizungumza katika mkutano wa wananchi uliofanyika viwanja vya ofisi ya Kijiji cha Lekura Dkt Kimei alisema anamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake mkubwa kwa wanaVunjo kwani serikali anayoiongoza imelipatia Jimbo hilo fedha nyingi za miradi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi na ukamilishaji wa zahanati hizo za Kimangara na Lekura hali itakayosogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi.



Dkt Kimei alisema katika mwaka huu wa fedha kupitia Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) watakwenda kuimarisha na kuboresha upatikanaji wa maji katika vijiji vinne vya Kiria, Kimangara, Kimbogho na Mkolowony kwa gharama ya shilingi milioni 180.


Kwa upande mwingine Dkt Kimei amesema amepokea kero ya mgogoro wa ardhi inayomilikiwa na ushirika wa KNCU katika Shamba la Mkolowonyi na Rauya ambayo atahakikisha anaifuatilia na kuhakikisha utatuzi unapatikana ili kuleta utulivu



Vile vile Dkt Kimei amewahakikishia wamiliki wa majengo katika soko la Kisambo mazungumzo juu ya mgogoro walionao na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi bado hayajafungwa hivyo waendelee kufanya biashara na kulipa mapato ya serikali huku namna bora zaidi ya ushirikiano baina yao na halmashauri ya Wilaya ya Moshi ikitafutwa kwa njia ya mazungumzo yatakayokuwa na faida kwa pande zote mbili. 


Amewahakikishia maboresho ya soko hilo ikiwemo ujenzi wa matundu nane ya choo katika soko hilo hali itakayoimarisha usalama wa afya kwa watumiaji mbalimbali wanaofika sokoni hapo. 



Diwani wa kata hiyo, Elirehema Tesha alisema kazi za maendeleo zilizofanyika katika kata hiyo ni nyingi na zinaonekana kwa macho ya nyama. 



Diwani Tesha alisema kata hiyo inakabiliwa na wimbi kubwa la wanyama waharibifu wakiwemo Tumbili na Nyani kuanzia kwenye mazao mashambani mpaka kwenye makazi ya wananchi hivyo kumuomba Dkt Kimei asaidie ili kuwaondolea wananchi kero hiyo. 


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kata hiyo, Eliakim Kimaro alisema tangu ujio wa vyama vingi hakuna mbunge ambaye aliwahi kuwafikia wananchi wa Mamba Kusini kwa kuwapelekea maendeleo kwa kiasi hicho kama Dkt Charles Stephen Kimei. 



Akizungumza na wananchi katika mkutano huo Mchungaji wa Usharika wa Lekura, Johansson Monyo alisema Dkt Kimei mwaka 2003 ndiye aliyewawezesha mtaji wa shilingi milioni 80 katika Saccos yao ya Tumaini iliyopo Lekura ambayo hali yake kwa sasa imeyumba sana na hivyo aliwasilisha ombi la kumtaka Dkt Kimei kusaidia ushauri wa kitaalam ili kuifufua na kusaidia ukusanyaji wa madeni angalau waliowekeza hisa zao wapate kulipwa fedha zao ambapo alipokea ombi hilo na kuahidi kulifanyia kazi. 


Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Samwel Mahanyu amesema katika kipindi cha miaka minne tangu wawakilishi wa CCM katika muundo wa mafiga matatu wachaguliwe katika nafasi zao wakiongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kazi kubwa ya maendeleo imefanyika katika kata ya Mamba Kusini na Jimbo la Vunjo kwa ujumla hivyo wananchi hawana sababu ya kuyumbishwa na siasa zisizo za maendeleo. 



Katika ziara hiyo iliyoanza na kikao cha ndani na ukaguzi wa mradi wa madarasa matatu shule ya msingi Kimbogho na matundu ya vyoo vya wanafunzi wakike, wakiume na walimu shule ya msingi Kikoro pamoja na kutembelea maeneo ambayo zahanati hizo za Kimangara na Lekura zitajengwa. 


Dkt Kimei aliambatana na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Wilaya ya Moshi Vijijini Andrew Mwandu, kamati ya maendeleo na kamati ya siasa kata hiyo pamoja na wataalam mbalimbali wa serikali.


Mwisho..

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI