Header Ads Widget

HALMASHAURI YA MBEYA KUTOA MIL.20 UBORESHAJI MADARASA S/M SHITETE, NJEZA AUNGA MKONO.

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Halmashauri ya Mbeya mkoani Mbeya, imetenga fedha shilingi million ishirini kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya vyumba viwili vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu katika shule ya msingi Shitete kata ya Isuto Mbeya vijijini ili kuwasaidia watoto kusoma katika mazingira safi na salama.


Kwa mujibu wa afisa mipango na uratibu wa Halmashauri ya Mbeya akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Serikali imefikia kutenga fedha hizo ili kuhakikisha shule hiyo inakuwa na vyumba vya kutosha kwa ajili ya watoto kusomea na uboreshaji mazingira yao kwa ujumla.

Kaimu mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Mbeya alipohojiwa na kituo hiki kuhusu mpango wa Serikali kuboresha shule hiyo hasa sakafu na madirisha, amesema tayari shilingi million ishirini zimetengwa na hivyo Serikali itahakikisha inakarabati vyumba viwili na ofisi ya walimu pamoja na kuweka madirisha ikiwa ni pamoja na kutengeneza uwanja wa shule kwa ajili ya michezo shuleni hapo.


Hayo yamejiri kufuatia ziara ya Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini anayoendelea naye katika Jimbo hilo kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi wake.

Alipofika shuleni hapo Mbunge Oran Njeza wa Mbeya vijijini, amesema atachangia shilingi million mbili kwa ajili ya kuunga mkono mpango wa Halmashauri kuboresha miundombinu ya shule hiyo ya msingi Shitete, huku akiahidi kuchangia shilingi laki mbili kwa ajili ya kuwaunga mkono wazazi na walezi kuhakikisha wanatoa chakula cha mchana shuleni kwa ajili ya watoto wao ikiwa ni mbinu ya kusaidia kuboresha ufaulu shuleni.


Aidha Mbunge huyo amemtia moyo mwalimu mmoja wa kujitolea shuleni hapo akimzawadia shilingi laki moja huku akitoa fedha watoto saba waliokutwa wakiwa hawana masweta kuhakikisha watoto hao wananunuliwa masweta.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Shitete Deogratius Sanga, amemshukuru Mbunge wa Mbeya vijijini kwa kutembelea shule hiyo akiamini safari hiyo ni ya neema kwa miundombinu kuboreshwa kama ilivyoahidiwa na viongozi mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI