Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA Poas Kilango (kushoto) akizungumza na viongozi wa CCM wilaya Kigoma Mjini walipotembelea mradi wa maji wa Kalalangabo
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kigoma vijiji, imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa chanzo cha maji cha Kibirizi katika manispaa ya Kigoma Ujiji ambacho kitawezesha kukabiliana na tatizo la uhaba wa maji lililokuwa likiwakabili wananchi wa kijiji cha kalalangabo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kigoma Mjini, Ahamed Mwilima alisema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo mradi huo wa chanzo cha maji unaotekelezwa na Mamlaka ya maji safi na maji taka Kigoma Ujiji (KUWASA) ikiwa ni kukagua ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mwilima alisema kuwa kwao kama chama wameshuhudia namna KUWASA ilivyoweza kutekeleza mradi huo kwa kugusa Maisha ya wananchi wa hali ya chini moja kwa moja ambapo mradi huo utaondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi 2000 wa Kijiji hicho.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira KUWASA Poas Kilangi amesema mradi huo ni matokeo ya kilio cha wananchi wa Kalalangabo walichofikisha ofisini kwake ili kutafutiwa ufumbuzi wa kero kubwa ya maji kijijini hapo ambapo Mamlaka hiyo ilianza kutafuta suluhu ya tatizo hilo.
Kilangi alisema kuwa awali chanzo hicho kilikuwa na changamoto ya usafirishaji wa maji kutokana na uwezo mdogo wa kufikisha majini kijijini hapo lakini kwa sasa wameongeza mashine ya kusukuma maji yenye uwezo mkubwa itakayowezesha kufikisha maji ya kutosha katika kijiji hicho baada ya kubadilisha chanzo ambapo kwa sasa chanzo hicho kinachukua maji kutoka chanzo cha Aman Beach mradi huo ukigharimu kiasi cha shilingi milioni 160.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kalalangabo akiwemo Stumai Maulidi wamepongeza hatua ya Mamlaka ya Maji Mafi na Usafi wa Mazingira KUWASA ya kutekeleza mradi huo ambao unaenda kutatua changomoto ya upatikanaji wa maji ya kipindi kirefu.
0 Comments