Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma
RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua jukwaa la ununuzi wa umma la Afrika mashariki litakalo fanyika Septemba 9 hadi 12 ,2024 mkoani Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Eliakim Maswi amesema kuwa hiyo ni mara ya nne kwa Tanzania kuratibu na kuandaa jukwaa hilo .
Mkurugenzi huyo amesema ufunguzi wa jukwaa hilo litaambatana na uzindizi wa mfumo wa ununuzi wa Kielektroniki (NeST) .
Amesema kuwa katika jukwaa hilo nchi za Afrika Mashariki zitashiriki ikiwemo Tanzania ambayo ndio mwenyeji, Kenya ,Uganda, Burundi ,Rwanda, Sudani ya Kusini , Somalia na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo.
"Jukwaa hili limekuwa likiendeshwa kwa zaidi ya miaka 14 sasa tangu lilipoandaliwa mwaka 2008 nchini Uganda ,ambapo tangu kuanza kwake Tanzania imekuwa ikishiriki kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA)" amesema.
Amesema jukwaa hilo linatarajiwa kukusanya washiriki wapatao 1000 kutoka katika nchi za Afrika Mashariki kwaajili yakujadili ajenda ya ununuzi wa umma katika eneo hilo.
"Washiriki hao watatoka katika sekta ya umma, sekta binafsi, mashirika ya kitaaluma,asasi za kiraia na taasisi za mafunzo na nyinginezo" amesema.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu huyo alitaja baadhi ya faida zinazopatikana kupitia jukwaa hilo kuwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano na ubadilishaji wa maarifa kati ya vyombo vya udhibiti wa ununuzi kutoka nchi wanachama wa Afrika Mashariki.
"Faida yingine ni pamoja na kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika utendaji kazi wa serikali kwa kuboresha mifumo ya kitaasisi na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa ununuzi ili kutekeleza majukumu na kazi zao kwa ufanisi kwa kuzingatia kanuni na viwango bora, " Amesema.
Na kuongeza " Lakini pia jukwaa linaipa PPRA na wadau wengine fursa ya kupata ujuzi na upasuaji habari ambao ni muhimu Kwa ajili ya kuendeleza uwazi na thamani ya fedha katika mikataba ya umma, " Amesema.
Pamoja na hayo ameeleza kuwa, tangu ulipoanza kutumika mfumo wa NeST julai 2023 mfumo huo umewezesha kupunguza muda wa michakato ya ununuzi wa umma,kupunguza gharama za michakato, kuziba mianya ya rushwa ,kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na usalama wa taifa za watumiaji.
0 Comments