Na Moses Ng'wat, Tunduma.
RAIS Samia Suluhu Hassan amesisitiza wananchi kuendelea kulipa kodi na tozo za serikali kwa kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Ametoa rai hiyo leo Julai 18, 2024 mjini Tunduma Wilayani Momba, Mkoani Songwe wakati akiwahutubia wananchi baada ya kusimama mjini hapo kwa lengo la kuwasalimia.
Rais Dkt. Samia alikuwa akiwasalimia wananchi wa Tunduma akiwa njiani kuelekea Dodoma Mara baada ya Kumaliza Ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
"Ni muhimu sana kulipa kodi kwani mazuri yote yaliyotajwa hapa na mema yote yaliyodaiwa serikali ifanye, tunafanya kutokana na fedha za kodi pamoja na fedha za tozo".
"Nakubali wakati mwingine wale tuliowaamini na kuwapa kazi ya kukusanya kodi wanafanya makosa hilo nalo tunaliangalia na tunarekebisha, lakini niwaomben sana ndugu zangu kila mmoja katika nafasi yake na biashara yake alipe kile anachopaswa kulipa". alisisitiza Rais Dkt. Samia.
Amesema miradi inayofanywa hivi sasa hapa nchini inatokana na fedha zinazokusanywa kwa njia ya kodi na tozo.
"Wakati mwingine fedha hizi hazitoshi na hadi tunaenda kukopa kwenye mashirika ya kimataifa na kutozwa riba kwenye mikopo hiyo, hivyo ili kuepuka hayo ni lazima tukusanye fedha zetu ndani" alisisitiza Dkt. Samia na kuomba wananchi kuendelea kulipa kodi na tozo za serikali.
Awali akihutubia wananchi katika jukwaa hilo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, alieza kuwa hali ya usalama katika mpaka wa imeimarishwa na kutoa fursa kwa watu kufanya shuhhuli za biashara kwa hali ya utulivu.
Aidha, Chongolo alitumia nafasi hiyo kuzungumzia changamoto ya msongamano katika mji huo wa mpakani wa Tunduma, hivyo kuomba utekelezaji wa mpango wa upanuzi wa barabara kutoka Igawa Mkoani Mbeya hadi Tunduma Mkoani kuanzia Tunduma.
Mwisho.
0 Comments