Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Mkazi wa Mjimwema Mjini Njombe Thadei Mbawala [48] Dereva wa gari za kampuni ya maji anadaiwa kukutwa akiwa amefariki ndani ya gari hilo pembeni kukiwa na jiko la mkaa.
Kituo hiki kimefika nyumbani kwa marehemu na kuzungumza na mkewe Catherine Haule ambaye anasema mumewe baada ya kurejea kazini majira ya usiku alimuaga kuwa anaenda kuchaji redio kwenye gari mpaka aliposhtuka asubuhi saa kumi na mbili na kukuta kajifungia ndani ya gari hilo.
Catherine amesema baada ya kutoa taarifa kwa majirani na polisi walipofika asubuhi walimkuta amejifunika blanketi akiwa amelala kwenye kiti cha gari.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mjimwema Theophil Mwinuka amesema imekuwa ni kawaida kwa marehemu huyo kwenda kuchaji redio ndani ya gari hilo lakini suala la kwenda na jiko la mkaa halijazoeleka.
Aidha Mwinuka amesema matukio ya watu kufa kwa moto wa mkaa sio mara ya kwanza katika kata yake kwani hata mwaka jana yaliripotiwa matukio ya aina hiyo.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Mjimwema akiwemo Shemeji wa Marehemu Gabriel Haule na Nolbert Mkalawa wanasema walipigiwa simu majira ya moja asubuhi kujulishwa kuwa ndugu yao hajatoka kwenye gari tangu usiku alipoenda kuchaji redio na milango imefungwa kwa ndani ndipo walipolazimika kufika nyumbani hapo.
Mara kwa mara jeshi la Polisi Mkoani Njombe kupitia Kamanda wake Mahamoud Banga limekuwa likitoa wito kwa wananchi kujiepusha kulala na majiko ya mkaa yakiwa na moto kwani ni hatari katika kipindi hiki cha baridi kali.
Hili ni tukio la 7 kuripotiwa kwa watu kufariki kwa moto wa mkaa katika kipindi cha miaka minne mkoani Njombe jambo ambalo wito unaendelea kutolewa kwa wananchi kuchukua tahadhari ya matumizi ya majiko ya mkaa katika kipindi cha baridi.
0 Comments