Matukio Daima App Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu amelisitiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha linakamilisha Mradi wa ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Wizara hiyo lililopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma katika muda uliopangwa kwenye makubaliano ya ujenzi wa mradi huo.
Gugu ametoa agizo hilo Julai 24, 2024 baada ya kukamilika kwa kikao kazi baina yake na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wizara ya Ujenzi Pamoja na Wakala wa Majengo (TBA) na baadaye kutembelea mradi huo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa jengo hilo
Katika ziara yake hiyo Katibu Mkuu, aliagiza kuwa ujenzi wa jengo hilo ukamilike ndani ya siku 66 zilizobaki ili kutimiza lengo na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha miradi mbalimbali inakamilika kwa wakati
“Mkataba huu unafikia ukomo kwa vile kukamilishwa unatakiwa kukamilika ifikapo Septemba 30, mwaka huu kwa hiyo kwa siku 66 zilizobaki bado kuna uwezekano wa kutimiza adhma na dhamira ya Serikali” Alisema Gugu.
“Pamekuwa na changamoto ya mradi huu kushindwa kukamilika kwa wakati kulingana na muda uliopangwa kimkataba, lakini kwa vile changamoto zilizojitokeza zilikuwa nje ya uwezo wa Wizara na mkandarasi ambaye ni NHC tuliweza kuongeza mkataba” Aliongeza
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah amesema licha ya kwamba mradi huo unakwenda vizuri, aliahidi kuukamilisha ujenzi huo kwa viwango ambavyo NHC imekubaliana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuongeza masaa ya kufanya kazi ili mradi huo ukamilike ndani ya siku zilizoagizwa
“Mimi kama kiongozi nitahakikisha timu yangu inafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha dhamira ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya kupata jengo zuri lenye viwango linatimia” Alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wizara ya Ujenzi Utawala na Rasilimaliwatu Mrisho Mrisho ambaye pia alimwakilisha katibu Mkuu wa Wizara hiyo, alisema Wizara itaendelea kuisimamia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ili ahadi iliyotolewa kwa katibu Mkuu iweze kutekelezwa kwa wakati
Awali, Msanifu Majengo, Victor Baltazar kutoka wakala wa majengo Tanzania (TBA) amesema Wakala wa Majengo Tanzania itatoa ushirikiano wa karibu na kutatua changamoto zote zilizosababisha mradi kusuasua na kuhakikisha kazi hiyo inakamilika ndani ya muda uliopangwa
Ziara hii ni muendelezo wa ziara ambazo zimekuwa zikifanywa na katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi inayolenga kufuatilia maendeleo ya mradi huo uweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango.
0 Comments