Na Thobias Mwanakatwe, IRAMBA
WANANCHI zaidi ya 4,192 wa kijiji cha Migilango wilayani Iramba mkoani Singida wataondokana na kero ya ukosefu wa maji safi na salama kufuatia kukamilika kwa mradi wa maji uliogharimu Sh.246,914,000 uliojengwa na wahisani.
Mradi huo umejengwa kwa ufadhiri wa Poul Due Jensen Grundfos Foundation ya nchini Denmark kupitia asasi isiyo ya kiserikali ya Water Gate Community Link ya Dar es Salaam kwa ushirikiano wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na kujengwa na mkandarasi wa kampuni ya BC Water Equipment Limited.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Iramba, Mhandisi Ezra Mwacha, akizungumza juzi wakati wa uzinduzi na kukabidhi mradi huo, alisema mradi huo utawezesha jamii kupunguza unyanyasaji wa kijinsia ambapo wanawake,watoto na wanafunzi ndio walikuwa wahanga wakubwa wa kutafuta maji.
Mwacha alisema manufaa mengine ya mradi huo utawezesha wananchi kuepuka maradhi yaliyokuwa yakisababishwa na ukosefu wa maji safi na salama,kupata maji karibu zaidi tofauti na mwanzo ambapo walikuwa wakilamika kutembea umbali wa kilometa 14 kufuata huduma ya maji.
Naye Mtendaji Mkuu wa asasi isiyo ya kiserikali ya Water Gate Community Link, John Mudende, alisema mradi huo utakuwa na ujazo wa lita 50,000 na kutakuwa na vituo vinne (DP) vya kuchotea maji wananchi wa kijiji hicho.
Alisema ili mradi uweze kukaa muda mrefu na kuendelea kutoka huduma ya maji kwa wananchi serikali,mamlaka za maji za wilaya na wananachi wahakikishe wanatunza miundombinu ya mradi isiharibiwe.
"Mradi huu umejengwa kwa fedha za wananchi wa huko duniani ambao walipambana na kuweka akiba ili sisi wananchi wa Tanzania hususani wa kijiji hiki cha Migilango waweze kupata maji na hivyo kwenda na sera ya serikali ya kumtua ndoo mama kichwani," alisema.
Mudende alisema wafadhiri wana utaratibu wa kutembelea miradi ambayo wametoa fedha hivyo haitakuwa jambo zuri watakapokuja wakute mradi umeharibika na hautoi maji.
Naye Meneja wa Tanzania wa Groundfos Foundation, Ngusa Breck, alisema ili miundombinu ya mradi huo iendelee kutunzwa, fedha ambazo zitakuwa zinakusanywa wakati wa kuuza maji zitunze kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya mradi huo utakapokuwa na changamoto.
Breck alisema changamoto kubwa ambayo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mengine baada ya mradi kuzinduliwa na maji kutoka lakini baada ya mwaka mmoja maji yanakuwa hayatoki na sababu kubwa inakuwa ni kutokuwa na fedha matengenezo ya miundombinu.
"Wafadhiri wakija wakakuta mradi hautowi maji maana yake wananchi wa kijiji cha Migilango mtakuwa wa kwanza kuzuia wananchi wa vijiji vingine kupata mradi wa maji,pia mtasababisha wadau wengine wanaosaidia miradi ya maji kuona Tanzania sio mahali salama pa kupeleka miradi ya maji," alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, akizunguma na wananchi baada ya kukabidhiwa na kuzindua mradi huo aliwashukru wafadhiri kwa kusaidia ujenzi wa mradi huo wa maji na kwamba utaongeza kiwango cha upatikanaji maji vijijini kufikia asilimia 68.
MWISHO
0 Comments